Yanga, Coastal zatishana

15Jan 2022
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Yanga, Coastal zatishana

IKIWA imebaki siku moja tu kabla ya mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara itakayochezwa kwenye Uwanja wa CCM Mkwakwani jijini Tanga kati ya wenyeji Coastal Union dhidi ya Yanga kutoka Dar es Salaam, kila upande umetamba kuibuka na ushindi katika mchezo huo.

Yanga itaingia kwenye uwanja huo ikiwa haijashinda mechi yoyote ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Wagosi wa Kaya hayo kwa misimu saba.

Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli aliliambia gazeti hili kwa sasa wao hawaishi kwa historia wala rekodi, na siku zote 'kuti la mazoea' ndilo humwangusha mgema.

Bumbuli alisema Coastal Union kwa sasa wamekuwa wakiishi maisha ya kukariri na historia, kitu ambacho wao hawakiamini, hivyo watashuka kwenye uwanja huo kusaka matokeo ya ushindi bila kufikiria matokeo mabaya wanayoyapata kwenye uwanja huo.

Katibu Mkuu wa Coastal Union, Rashid Mgwemo alisema ana uhakika wa kuibuka na ushindi kutokana na historia yao nzuri wanapocheza dhidi ya Yanga nyumbani kwao.

"Mechi itakuwa nzuri na ngumu. Sio siri kuwa Yanga msimu huu ni nzuri na ina wachezaji wazuri, lakini ikumbukwe msimu uliopita tuliwafunga Mkwakwani, tukiwa hatuna timu nzuri kama msimu huu. Kwa hiyo na sisi msimu huu tuna timu nzuri kuliko hata ya msimu uliopita, waje vizuri tu," Mngweno alionya.

Habari Kubwa