Yanga dimbani ikiiwaza Simba

27Jun 2020
Somoe Ng'itu
Dar es Salaam
Nipashe
Yanga dimbani ikiiwaza Simba
  • ***Ni katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Ndanda leo, huku Azam ikiwa ugenini Musoma...

WAKATI safari ya kuwania taji la Ligi Kuu Tanzania Bara ikielekea ukingoni, vinara wa ligi hiyo, Simba wanaweza kutawazwa mabingwa wapya endapo Yanga na Azam FC watapoteza mechi zao za wakiwa kwenye viwanja tofauti hapa nchini.

Kocha Mkuu wa Yanga, Luc Eymael:PICHA NA MTANDAO

Yanga itawakaribisha Ndanda FC kwenye Uwanja wa Taifa jijini, Dar es Salaam wakati Azam FC iliyoko Musoma mkoani Mara itawavaa wenyeji Biashara United.

Yanga yenye pointi 57 ikishinda mechi ya leo, na michezo mingine sita itakayofuata, itafikisha pointi 78 wakati Azam wenyewe wakishinda mechi zote zilizosalia watafikisha pointi 79, wakati Simba inayoongoza ligi ina pointi 78 mkononi.

Katika mechi ya leo, Yanga itaendelea kuwakosa wachezaji wake wa kimataifa wawili, Bernard Morrison na Lamine Moro, ambao wamefungiwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kutokana na makosa tofauti.

Akizungumza na gazeti hili, Kocha Mkuu wa Yanga, Luc Eymael, alisema kila mechi kwao ni sawa na fainali na watashuka uwanjani leo kuikaribisha Ndanda wakiwa na mipango tofauti.

"Kuna makosa mbalimbali tumefanya katika mechi zetu tatu zilizopita, lakini kesho (leo), tutakuwa tofauti, tunahitaji pointi tatu tu na si matokeo mengine, nina matumaini tutapata ushindi, ili tutimize malengo yetu," Eymael alisema.

Naye Ofisa Mhamasishaji wa timu hiyo, Antonio Nugaz, amewataka mashabiki wa Yanga wawe na subira na kuendelea kuishangilia timu yao ili ipate ushindi ili kuendelea kuwania nafasi ya pili wanayoifikiria.

"Tayari mwalimu wetu, (Eymael) ameshayafanyia kazi matatizo na namna timu itakavyokuwa inapata magoli, licha ya changamoto zilizojitokeza katika mechi mbili zilizopita, tuungane kwa pamoja," Nugaz alisema.

Kocha wa Ndanda, Abdul Mingange, aliliambia gazeti hili kikosi chake kitaingia uwanjani kuwakabili Yanga tahadhari ili kuondoka na pointi.

Mingange alisema katika mechi hiyo kila upande inataka matokeo na wamekuwa na ushindani kila wanapokutana kuanzia timu yake ilipopanda daraja.

Aliongeza wachezaji wa Yanga hawakati tamaa hadi mwisho wa mchezo, hivyo wataingia uwanjani wakiwa makini zaidi.

"Mimi na wachezaji wangu tumeshazungumza tunahitaji pointi, katika mechi hizi tatu tunahitaji hata pointi moja, tunajua Yanga pia inahitaji hata pointi moja, tunawaheshimu na tunafahamu ni timu kubwa, ina wachzeaji wazuri na wanaolipwa vizuri," Mingange alisema.

Kipa wa Ndanda FC, Ally Mustapha, alisema timu yao inaundwa na wachezaji mchanganyiko, hivyo wataingia uwanjani wakiwa na malengo ya kusaka ushindi tu.

"Ni timu kubwa, tunawaheshimu Yanga na wakiwa nyumbani wana faida yao, tunawaheshimu lakini Jumamosi tutaingia kusaka matokeo," Barthez, kipa wa zamani wa Simba na Yanga alisema.

Mechi nyingine za Ligi Kuu Bara zitakazochezwa leo ni Ruvu Shooting itakayowakabili Namungo wakati Alliance itawavaa Coastal Union huku Mwadui ikiwapokea Mtibwa Sugar na Mbeya City itapambana na JKT Tanzania.

Kagera Sugar ambayo msimu huu imezinduka mapema itawakaribisha KMC FC ambayo iko kwenye hatari ya kushuka daraja endapo itaendelea kuvurunda.

Habari Kubwa