Yanga, Esperanca vita kali

07May 2016
Somoe Ng'itu
Nipashe
Yanga, Esperanca vita kali
  • ***Wanajangwa wana kila sababu ya kutumia vizuri uwanja wa nyumbani kupata ushindi mnono dhidi ya timu hiyo ya Angola katika mechi kwanza – mtoano Kombe la Shikisho…

WA-KIMATAIFA Yanga, leo wanaendelea na kampeni yao ya kusaka taji la kimataifa Afrika watakapoikaribisha Sagrada Esperanca ya Angola katika mechi ya kwanza ya mtoano ya kuwania kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

kikosi cha yanga

Yanga inawakaribisha wageni hao ikiwa na rekodi ya kushinda mechi tatu za kwanza za kimataifa (Cercle de Joachim ya Mauritius 3-0 nyumbani na 1-0 ugenini, halafu ikawafunga APR ya Rwanda ugenini mjini Kigali mabao 2-1 na kupata sare ya 1-1 waliporejeana Dar es Salaam.

Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu ya Bara pia walitoka sare ya 1-1 dhidi ya Al Ahly ya Misri na kukubali kipigo cha magoli 2-1 na kutolewa kwenye michuano ya Klabu Bingwa Afrika.

Kikosi cha Sagrada kilichoanzishwa Desemba 22, 1976, kiliwasili nchini juzi usiku na kitashuka uwanjani kikiwa na kumbukumbu nzuri ya kupata ushindi wa jumla wa mabao 4-1 (ilishinda 2-1 ugenini na ikawafunga 2-0 V. Club Mokanda ya Kongo katika mchezo wa marudiano wakiwa nyumbani kwao katika mechi zake mbili za mwisho.

Waangola hao walianza kampeni kwa kufungwa na Ajax Cape Town ya Afrika Kusini mabao 2-1 ugenini na kushinda 2-0 nyumbani, huku ikiwafunga LD Maputo ya Msumbiji 1-0 na marudiano wakitoka sare ya 1-1.

Katika mechi ya leo, Yanga itawakosa wachezaji wake wawili wa kimataifa kutoka Zimbabwe Donald Ngoma na Thaban Kamusoko ambao wanatumikia adhabu ya kadi mbili za njano.

Kocha Mkuu wa Yanga, Hans van der Pluijm alisema mechi ya leo ni zaidi ya fainali, lakini anaamini umuhimu wa uwanja wa nyumbani utawasaidia.Pluijm alisema kukosekana kwa Ngoma ni pigo kwenye kikosi chake.

"Wachezaji wote wamefanya mazoezi, hakuna majeruhi, hadi sasa sijafahamu nani atacheza nafasi ya Ngoma," alisema kwa kifupi kocha huyo baada ya kumaliza mazoezi jana asubuhi kwenye Uwanja wa Taifa.

Nahodha wa Yanga, Nadir Haroub 'Cannavaro' alisema hakuna mechi rahisi katika mashindano hayo na hatua hiyo waliyofikia wapinzani wao inaonyesha ni moja ya timu yenye wachezaji wenye uzoefu.

Cannavaro alisema kuwa wanatarajia kutumia vyema uwanja wa nyumbani ili kujitengenezea mazingira ya kusonga mbele kwenye michuano hiyo.

"Tunazidi kumuomba Mungu tufanye vizuri, tunawaahidi Wanayanga na Watanzania hatutawaangusha," Cannavaro alisema.
Refa Joseph Odartei Lamptey kutoka Ghana ndiye atachezesha mchezo huo akisaidiana na David Laryea na Malik Alidu Salifu wakati Kamisaa ni Asfaw Luleseged Begashaw kutoka Ethiopia.

Habari Kubwa