Yanga: Hatutapaki ‘basi’ Kigali

10Mar 2016
Somoe Ng'itu
Dar
Nipashe
Yanga: Hatutapaki ‘basi’ Kigali

KOCHA wa Yanga, Hans van der Pluijm, amesema hatatumia falsafa ya kupaki ‘basi’ watakapowakabili wenyeji wao, APR ya Rwanda katika mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika Jumamosi hii mjini Kigali.

Kocha wa Yanga, Hans van der Pluijm.

Badala yake, amesema ushindi ugenini ni muhimu hivyo, kikosi chake kitacheza soka la kushambulia na kujiamini, lengo likiwa ni kupata ushindi na kujiweka kwenye nafasi nzuri katika mechi ya marudiano ndani ya wiki mbili zijazo.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Pluijm alisema wana dhamira moja tu, nayo ni kupata ushindi mnene ugenini. Ili kuhakikisha ushindi unapatikana, Pluijm alisema atatumia muungano wake hatari wa safu ya ushambuliaji; Simon Msuva, Amissi Tambwe na Donald Ngoma (MTN).

Pia atawajaza nguvu washambuliaji kwa kuwaruhusu mabeki wake kupanga langoni mwa wapinzani wao na kufanya mashambulizi.

“Kwa mfumo huu, muda mwingi tutakuwa tunashambulia na unaposhambulia mfululizo, maana yake tunatengeneza nafasi nyingi za kufunga, ambazo lazima tuzitumie,” alisema Pluijm.

Katika mechi hiyo, Yanga itamkosa nahodha, Nadir Haroub 'Cannavaro', ambaye amepata nafuu kutoka kuwa majeruhi, lakini siyo kwa ajili ya mechi. Hata hivyo, pengo hilo siyo tatizo kwa Pluijm:

“Nafurahishwa na safu ya ulinzi, inafanya vizuri, naamini [Pato Ngonyaji] ataziba vizuri pengo la nahodha wake akishirikiana na Kelvin Yondani na Vicent Bossou.

” Kuhusu wapinzani wao, alisema ameangalia mechi zao kadhaa, hivyo anajua jinsi ya kuwakabili kwenye mchezo huo. Kikosi hicho kinatarajia kuondoka leo asubuhi kuelekea Kigali, Rwanda tayari kwa mchezo huo.

Habari Kubwa