Yanga: Iringa ngome ngumu kwetu 2018/19

22May 2019
Somoe Ng'itu
DAR
Nipashe
Yanga: Iringa ngome ngumu kwetu 2018/19

WAKATI msimu wa Ligi Kuu Bara 2018/19 ukielekea ukingoni, Klabu ya Yanga imeutaja mkoa wa Iringa kuwa ni ngome ngumu kwao na watajipanga kuhakikisha mwakani hawapati tena matokeo mabaya.

Mratibu wa Yanga, Hafidh Saleh

Yanga ilipoteza mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Lipuli FC na pia ikakubali kufungwa na wenyeji hao katika mechi ya hatua ya nusu fainali ya Kombe la FA.

Akizungumza na Nipashe jana, Mratibu wa Yanga, Hafidh Saleh, alisema kuwa msimu huu wamekutana na changamoto mbalimbali, lakini bado wataikumbuka Lipuli FC kwamba ni klabu iliyowasumbua sana.

Saleh alisema pia changamoto nyingine waliyokutana nayo msimu huu unaoelekea mwishoni ni suala la fedha za uendeshaji na hili lilikuwa ni tatizo la klabu nyingi zilizoshiriki ligi hiyo yenye timu 20 kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini.

"Tunashukuru hadi hapa tulipofika, mambo hayakuwa rahisi sana, lakini tulijitahidi kupambana kusaka ushindi katika kila mechi tuliyocheza, changamoto ni sehemu ya mpira, lakini mkoa wa Iringa haukuwa mwepesi kwetu, wametufunga katika ligi na kututoa kwenye FA, ni matokeo mabaya sana, hatukuyatarajia," alisema kiongozi huyo.

Aliwashukuru mashabiki na wanachama wa timu hiyo kwa kuwachangia fedha na michango yao iliyosaidia katika kuwafikisha hapa walipo ambapo ni nafasi ya pili katika msimamo wa ligi hiyo inayotoa mwakilishi wa Tanzania Bara katika mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika kila mwaka.

Yanga inaendelea na mazoezi yake chini ya Kocha Mkuu, Mwinyi Zahera, na leo itashuka Uwanja wa Uhuru kuwakaribisha Mbeya City kutoka jijini Mbeya.

Baada ya mchezo huo, Yanga wataendelea kujiimarisha na kujipanga vema ili kuwavaa mabingwa wa Kombe la Kagame, Azam FC katika mechi ya mwisho wa msimu itakayochezwa Jumanne ijayo kwenye Uwanja wa Uhuru jijini.

Mechi hiyo itakuwa ni ya kusaka heshima kwa kila upande baada ya klabu hizo mbili kupoteza matumaini ya kutwaa ubingwa wa msimu huu.

Habari Kubwa