Yanga, Kagera mechi ya kisasi

30Jun 2020
Saada Akida
Dar es Salaam
Nipashe
Yanga, Kagera mechi ya kisasi

KOCHA Mkuu wa Yanga, Luc Eymael, amesema wanahitaji kulipa kisasi katika mechi ya hatua ya robo fainali ya Kombe la FA dhidi ya Kagera Sugar inayotarajiwa kuchezwa leo kwenye Uwanja wa Taifa jijini, Dar es Salaam.

Yanga itashuka katika mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya kichapo cha mabao 3-0, walichopata mara ya mwisho wakipokutana kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara.

Akizungumza na gazeti hili jijini jana, Eymael alisema anaandaa kikosi cha ushindi na anaamini wako tayari kulipa kisasa kwa kuwaondoa Kagera Sugar katika mashindano hayo.

Eymael alisema hataki kupoteza mechi hiyo na hawako tayari kumbukumbu ya kichapo kutoka kwa timu hiyo ijirudie katika mchezo huo ambao utawasaidia kuendelea na safari ya kusaka nafasi ya kuiwakilisha nchi kwenye michuano ya kimataifa.

Alisema anawaheshimu Kagera Sugar ni timu yenye wachezaji wazuri na wataingia uwanjani kupambana kutafuta matokeo chanya katika mchezo wao huo  utakaokuwa wa ushindani kwa pande zote.

"Hii ni mechi ngumu sana kwa pande zote mbili, binafsi tunahitaji kulipa kisasi pia kuhitaji kucheza nusu fainali ili tuje kucheza fainali ya FA michuano ya FA ndio itatuongoza kushiriki michuano ya kimataifa, tuko makini," alisema Eymael.

Kocha huyo pia aliipongeza Simba kwa kutetea ubingwa kwa mara ya tatu mfululizo na kueleza kikosi hicho kilistahili kutwaa kombe hilo.

"Simba, Kagera wameonyesha mpira mzuri wa wachezaji kucheza vizuri, tofauti na mechi zetu za hivi karibuni, nina kazi katika mchezo dhidi ya wapinzani wetu wa FA, kwani waliwahi kutusumbua," alisema Eymael.

Mechi nyingine ya robo fainali ya michuano hiyo itakayochezwa leo itakuwa ni kati ya Sahare Stars dhidi ya Ndanda FC kwenye Uwanja wa CCM Mkwakwani jijini Tanga.

Habari Kubwa