Yanga kamili yapaa Mauritius

12Feb 2016
Somoe Ng'itu
Dar es Salaam
Nipashe
Yanga kamili yapaa Mauritius
  • ***Inakwenda kucheza mechi yake ya kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Cercle de Joachim...

SAFARI imeiva. Wawakilishi wa Bara Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga wanatarajia kuondoka alfajiri kuelekea Mauritius na kesho wanashuka dimbani kukipiga na wenyeji wao, Cercle de Joachim.

BAADHI YA WACHEZAJI WA YANGA

Yanga inaondoka nchini, huku ikiwa inaongoza msimamo wa Ligi Kuu ya Bara baada ya ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya JKT Ruvu Jumapili iliyopita.

Kocha Mkuu Yanga Mholanzi, Hans van der Pluijm alisema wachezaji wake wako kamili kwa ajili ya mechi hiyo.

Pluijm alisema ni lazima kushina mchezo huo wa ugenini ili iwe rahisi kwako kwenye mechi ya marudiano Dar es Salaam.

"Tutashambulia kulingana na nafasi tutakazopata, lakini pia lazima tutakuwa makini muda wote wa mchezo, hakuna kufanya makosa kama tunahitaji ushindi," alisema Pluijm.

Alisema wanakwenda ugenini wakiwa na tahadhari kwa sababu wanaamini wapinzani wao nao watakuwa wamejipanga kupata ushindi wakiwa kwenye uwanja wa nyumbani.

"Hakuna timu ndogo, tutaingia uwanjani kwa ajili ya kupambana na siyo kuwaza ukubwa wa wapinzani wetu. Mara nyingi ninawakumbusha wachezaji kuzingatia hilo," alisisituza Pluijm.

Meneja wa timu hiyo, Hafidh Saleh alisema wanaondoka na ndege ya kukodi wakiwa na wachezaji 24.

Saleh alisema kuwa hakuna mchezaji mgonjwa wala majeruhi, hivyo wana uhakika wa kufanya vizuri kwenye mechi hiyo.
Kikosi cha Yanga kilifanya mazoezi ya mwisho jana kwenye Polisi Kurasini.

Timu hizo zitarudiana Februari 27 kwenye Uwanja wa Taifa na mshindi atakutana na kati ya APR ya Rwanda au Mbabane Swallows ya Swaziland.

Habari Kubwa