Yanga kazi ile ile kwa Kagera Sugar

13Nov 2022
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Yanga kazi ile ile kwa Kagera Sugar
  • Yajipanga kufikisha mechi 46 bila kupoteza leo, Nabi asema wamejipanga…

WAKIWA bado na furaha waliyoipata baada ya kuichapa Club Africain bao 1-0 ugenini nchini Tunisia na kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho la soka Afrika, CAF, Mabingwa Watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara Yanga, leo watashuka kwenye Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza kucheza dhidi ya Kagera Sugar-

-ambao ni wenyeji wa mechi hiyo.

Mechi hiyo itachezwa ikiwa ni siku nne tu tangu ilipocheza mechi hiyo ya mchujo kwenye jiji la Tunis na kuandika historia ya kutinga hatua ya makundi ya kombe hilo baada ya misimu minne.

Kocha Mkuu wa timu hiyo, Nasreddine Nabi amesema wanakwenda kucheza mechi ngumu kwani tangu Kagera Sugar ilipobadilisha mwalimu imeonekana kuimarika.

Nabi pia alilalamikia uchovu wa wachezaji wake akisema wametumia muda mrefu wakiwa angani kuliko ardhini.

"Katika kila mechi ya timu kubwa kama Yanga ni kujiandaa kikamilifu na kumheshimu mpinzani unayekwenda kucheza naye. Tumejiandaa na mechi hii ingawa ni kwa shida sana kwani tumetumia muda mrefu kwenye ndege kuliko kwenye ardhi, hilo ni tatizo kwa afya ya wachezaji, mchoko, lakini hatujaja hapa kulalamika, tumejiandaa na mechi tuna deni kwa mashabiki wetu.

“Tutoe wito kwa viongozi wenye mamlaka, sisi tumekwenda kuiwakilisha Tanzania, tusiadhibiwe kwa hili, tunaamini hili halitojitokeza tena," alisema Nabi.

Yanga ambayo si tu kwamba ndiyo timu pekee ambayo haijapoteza mechi yoyote msimu huu hadi sasa, lakini haijapoteza michezo 45 hivyo kama itapata ushindi au kutoka sare itafikisha mechi 46 na kuzidi kutengeneza rekodi ya aina yake.

Itakuwa ni mechi ya tisa kwa Yanga ambayo ina pointi 20 hadi sasa na kabla ya mechi ya Simba dhidi ya Ihefu iliyochezwa jana usiku, ilikuwa ikiongoza ligi.

Hata hivyo, itakuwa ni mechi ya 11 kwa Kagera Sugar ambayo kwa sasa ipo chini ya Mecky Mexime baada ya hivi karibuni kumtimua kocha wake Mkenya, Francis Baraza kutokana na mwenendo mbaya wa timu.

Akizungumzia mechi hiyo, Mexime alisema mechi itakuwa ngumu kwa sababu wanacheza na timu ambayo wachezaji wake wanatembea na matokeo miguuni.

"Mchezo utakuwa mgumu, tumejipanga na tunazitaka pointi tatu, kuhusu mambo ya kiufundi sitowapa nyinyi ila nitawapa vijana wangu.

“Ukicheza na timu hizi kama za Simba au Yanga ambazo wachezaji wake wanatembea na matokeo kwenye miguu yao, lakini ucheze kwa tahadhari sana. Nawapa hongera sana Yanga wamecheza na 'Waarabu' wameupiga mwingi, lakini sasa waje huku wakutane na 'waswahili' wenzao, sisi hatuna majeruhi, wachezaji wote wapo vizuri na tumesafiri na wachezaji wote kutoka Kagera," amesema Mexime.

Timu hiyo ipo kwenye nafasi ya 12 kwa pointi zake 11, hivyo inahitaji kuondoka eneo hilo na kusogea juu kidogo.

Habari Kubwa