Yanga kila nafasi bao leo

09Apr 2016
Na Waandishi Wetu
Dar
Nipashe
Yanga kila nafasi bao leo
  • ***Kocha wawakilishi hao wa Tanzania, amewakata wachezaji wake kutikisa kamba za Al Ahly kwa kila nafasi watakayopata uwanjani...

PIGA ua ushindi leo lazima. Ni maneno unayoweza kuyazungumza kuelekea mechi ya pekee na aina yake raundi ya pili Ligi ya Mabingwa Soka Afrika, kati ya Yanga na mabingwa wa kihistoria wa michuano hiyo, Al Ahly ya Misri.

Yanga haitapaswa kuwa na matokeo mbadala zaidi ya ushindi mnono wakatapowakaribisha Waarabu hao kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ambako macho na masikio ya wapenda soka yataelekezwa.

Wawakilishi hao wa Tanzania wanashuka dimbani wakiwa na jeraha la kuondolewa na timu hiyo kwenyes mashindano hayo mwaka 2014 kwa mikwaju ya penalti 4-3 baada ya upande kushinda nyumbani 1-0.

Hata hivyo, wachezaji watano wa kikosi cha kwanza kilichoanza cha mabingwa hao Bara na kushinda 1-0 mwaka juzi, leo hawatakuwa.

Haruna Niyonzima anasumbuliwa na homa ya malaria. Wengine watakaokosekana ni Emmanuel Okwi, Mrisho Ngasa, Frank Domayo na Hamisi Kiiza.

Kocha wa Yanga, Hans van der Pluijm, alisema anajivunia utayari wa wachezaji wake kuelekea mchezo huo.
Pluijm alisema kama wachezaji wake watafuata maelekezo aliyotoa wakati wa maandalizi, hapana shaka wataibuka na ushindi kwenye mechi hiyo.

"Yanga ina tatizo kubwa la kutengeneza nafasi nyingi za kufunga bila kuzitumia. Nimewaeleza kila mmoja awe makini, nafasi moja - bao moja," alisema Pluijm.

Aliongeza: "Lazima tushambulie na kulinda lango pia, wapinzani wetu hawapaswi kusongelea lango letu na mashambulizi."
Aliongeza kuwa mbali na kuwategemea washambuliaji wake watatu tegemeo ambao ni Simon Msuva, Amissi Tambwe na Donald Ngoma, pia atawatumia mabeki wake, Juma Abdul na Haji Mngwali kushambulia na kulinda lango.

Al Ahly ilitua nchini Jumatano na kufanya mazoezi yake kwenye Uwanja wa Gymkhana na kukataa kuzungumza lolote kuhusiana na mechi hiyo.

Katika mchezo huo, Yanga lazima wawe makini na mshambuliaji hatari wa timu hiyo, Ramadan Sobhi ni bingwa wa kutumia vizuri nafasi anazopata uwanjani.

Yanga ilitinga raundi hiyo ya pili baada ya kuifunga APR ya Rwanda jumla ya magoli 3-2, wakati Al Ahly iliyotoka suluhu ugenini Angola iliwafunga 2-0 nyumbani kwake Recreativo do Libolo.

Wakati huohuo, Jeshi la Polisi Kanda Maalamu ya Dar es Salaam limepiga marufuku wapenzi na mashabiki wa mpira nchini kuingia uwanjani na aina yeyote silaha wala chupa za maji kwenye mechi ya Yanga na Al Ahly.

Kauli hiyo imetolewa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalamu ya Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jana.

Alisema jeshi hilo limejipanga kuhakikisha mchezo huo unafanyika kwa usalama.

“Mageti yote ya kuingia na kutoka yatafungwa kamera kwa ajili ya kurekodi matukio yanayotokea uwanjani,” alisema.

Imeandikwa na Somoe Ng'itu na Na Leonce Zimbandu

Habari Kubwa