Yanga kuiwekea kambi Simba SC Mauritius

09Feb 2016
Sanula Athanas
Dar es Salaam
Nipashe
Yanga kuiwekea kambi Simba SC Mauritius

HOMA ya mechi ya watani wa jadi imezidi kuongezeka baada ya Yanga kuamua kuweka kambi ya siku 10 nchini Mauritius, Nipashe inathibitisha.

Salum Telela wa Yanga (aliyenyoosha mguu) na kipa wa JKT Ruvu, Shaban Dihile

Kikosi cha Wanajangwani chenye nyota 21 kitaondoka kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam kesho alfajiri kwenda Mauritius kwa ajili ya mechi ya mwishoni mwa wiki dhidi ya klabu ya Cercle de Joachim, lakini hakitarejea nchini baada ya mechi hiyo ya kwanza ya hatua ya awali ya Klabu Bingwa Afrika. Chanzo chetu ndani ya klabu hiyo kilieleza jana kuwa kikosi chao kitaweka kambi maalum nchini Mauritius kwa ajili ya 'dozi' ya Simba na kitarejea nchini siku moja kabla ya mechi ya pili ya watani wa jadi msimu huu ambayo itachezwa kwenye Uwanja wa Taifa Februari 20. "Msafara wetu utakuwa na watu 31, tunakwenda na wachezaji 21. Ni karibu nyota wetu wote kwa ajili ya msimu huu isipokuwa (Benedict) Tinoco, (Geofrey) Mwashiuya na Matheo (Antony)," chanzo chetu kilieleza. "Tinoco ni kipa na tunatakiwa kwenda na makipa wawili, Mwashiuya na Matheo 'passport' (hati za kusafiria) zao hazijapatikana kwa wakati." Nipashe inafahamu kwamba Ayubu Nyenzi, mjumbe wa kamati ya utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ndiye atakayeongoza msafara wa watu 31 wa Yanga utakaoondoka Dar es Salaam kesho alfajiri ukitua Afrika Kusini kabla kuunganisha ndege kwenda Mauritius. Alipotafutwa na gazeti hili jijini Dar es Salaam kuzungumzia suala hilo, Jerry Muro, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Yanga, hakuwa tayari kuzungumzia wala kukanusha taarifa za kambi yao ya Mauritius. Lakini uongozi na benchi la ufundi la Yanga wanafahamu fika juu ya ubora wa Simba. Timu hiyo imeshinda mechi zote sita (tano za Ligi Kuu) chini ya kocha mkuu wa muda, Jackson Mayanja. Wanafahamu pia kuwa wapinzani wao wa jadi si tu wanahitaji kulipa kisasi cha mabao 2-0 mzunguko wa kwanza, bali pia wanataka kuifunga Yanga ili rahisi kwao kumaliza ukame wa miaka minne bila taji la Ligi Kuu Msimbazi. Huku akikiri joto la mechi ya Februari 20 limeshaanza kumsumbua, kocha wa Yanga, Hans van Pluijm jana alisema: "Hakuna haja kufikiri sana kuhusu mechi dhidi ya Simba kwa sasa wakati tuna mchezo muhimu wa kimataifa kabla ya kukutana nao (Simba). Ninataka wachezaji wangu kuelekeza akili zao kwenye mchezo wa Mauritius."

Habari Kubwa