Yanga kukabidhiwa kikombe Mtwara

10May 2016
Somoe Ng'itu
Nipashe
Yanga kukabidhiwa kikombe Mtwara
  • ...Sherehe hizo zitafanyika Jumamosi baada ya mechi dhidi ya Ndanda FC itakayofanyika kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona...

UONGOZI wa Yanga umesema kuwa watasheherekea ubingwa wao baada ya mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Ndanda FC itakayofanyika Jumamosi mkoani Mtwara imeelezwa jana.

Yanga yenye pointi 68 ilitangazwa mabingwa wapya wa msimu 2015/16 juzi baada ya mahasimu wao Simba kupata kichapo cha goli 1-0 kutoka kwa Mwadui FC katika mechi ya ligi hiyo iliyofanyika kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mkurugenzi wa Bodi ya Ligi Tanzania, Boniface Wambura Mgoyo alisema kuwa mchakato wa kuwapa Yanga kikombe haukuweza kumalizika mapema na hivyo kuamua kuwakabidhi kombe baada ya mechi dhidi ya Ndanda.
"Baada ya jana (juzi) kutwaa ubingwa, muda wa maandalizi ya kuwapa kikombe ulikuwa mdogo, tumeshindwa kukamilisha na tukio hilo litafanyika Mtwara kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona," alisema Wambura.

Baada ya Simba kutoka sare juzi, tayari Yanga ilitetea ubingwa wake kutokana na kutokuwa na timu nyingine itakayofikisha pointi 68 hata ikishinda mechi zake zilizobakia.

Simba yenye pointi 58 baada ya kucheza mechi 27 inaweza kufikisha pointi 67 ikishinda mechi zake zote tatu zilizobaki, wakati Azam FC inaweza kumaliza na pointi 66.

Habari Kubwa