Yanga kukamilisha usajili wiki mbili

29Jul 2021
Saada Akida
Dar es Salaam
Nipashe
Yanga kukamilisha usajili wiki mbili

UONGOZI wa Yanga sasa umeelekeza nguvu zake katika kuimarisha kikosi na wanatarajia ndani ya wiki mbili watakuwa wamekamilisha usajili wa kikosi cha timu hiyo, kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara na michuano ya kimataifa.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mshauri wa Yanga, Senzo Mazingiza alisema baada ya kurejea kutoka Kigoma walikuwa na kikao viongozi wote wa kamati ya utendaji kwa lengo la kukamilisha usajili wa wachezaji wapya.

Alisema uongozi umejipanga vizuri na ndani ya wiki ijayo kikosi cha Yanga kitakuwa imara kulingana na kukamilisha usajili wa wachezaji wapya na kuungana na wenzao kurejea kambini mapema.

"Uongozi umejipanga vizuri, ndani ya siku hizi chache tutakamilisha usajili wa wachezaji wapya, zoezi la usajili linaendelea ili kuhakikisha nyota wapya wanakuwa sehemu ya kikosi kuelekea michuano ya Kagame," alisema mshauri huyo.

Alisema wako makini katika usajili wa ndani na nje, kulingana na mahitaji yao kuelekea msimu ujao kwa kufanya vizuri katika michezo ya Ligi Kuu na michuano ya kimataifa.

"Muda ni mchache tunatakiwa, kukamilisha usajili mapema kabla ya Agosti 15, tuna kazi ya kufanya na tuko makini hadi wiki ijayo tukamilishe usajili kwa asilimia kubwa," alisema Senzo.

Alisema kuwa na kikosi imara kwa msimu ujao kulingana na jinsi ya mapendekezo ya benchi lao la ufundi chini ya kocha wao Nesreddine Nabi kwa ajili kuboresha kikosi chao kulingana na mahitaji ya msimu ujao.

Mshauri huyo alisema wanatarajia wachezaji wapya kuanza kuonekana katika michuano ya Kombe la Kagame itakayoanza kutimua vumbi Agosti Mosi mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Katika michuano hiyo Yanga imethibitisha kushiriki ikiwa ni miongoni mwa timu za nchi sita ambazo zitacheza michuano hiyo huku ikiwa imepangwa kundi C ambalo kuna Yanga, Nyasa Big Bullets (Malawi) na Express FC (Uganda).

Kundi B kuna AZAM FC (Tanzania), Atlabara (Sudan Kusini), Tusker (Kenya) na Kundi A kutakuwa na KCCA (Uganda), Le Messanger Ngozi FC (Burundi) na KMKM FC (Zanzibar)