Yanga kula sahani moja na Asukile

04May 2021
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Yanga kula sahani moja na Asukile

KLABU ya Yanga imesema itachukua hatua kali kwa mchezaji Benjamin Asukile, endapo akishindwa kuthibitisha madai yake kuwa kuna baadhi ya viongozi waliowapigia simu baadhi ya wachezaji wa Tanzania Prisons kwa madai ya kutaka kutoa pesa kiasi cha Sh. milioni 40 ili wacheze chini ya kiwango kwenye-

Benjamin Asukile.

-mechi ya hatua ya 16-bora ya Kombe la FA lililochezwa Ijumaa iliyopita katika Uwanja wa Nelson Mandela mjini Sumbawanga na wa 'Wajelajela' hao kupigwa bao 1-0.

Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli, amesema kuanzia jana walikuwa kwenye harakati za kuziandikia mamlaka husika kutaka mchezaji huyo ahojiwe na apeleke ushahidi ili hatua zichukuliwe kama kuna baadhi ya watu walihusika na hilo na kama alikuwa anaongea kwa kuichafua klabu ya Yanga, basi watachukua hatua za kisheria dhidi yake.

"Sisi tumemsikia, ni kauli inayoelekea kuichafua klabu yetu ya Yanga, anataka kuonyesha kuwa sisi tusingeweza kuishinda timu yao bila kuwatafuta. Yaani timu yao ni bora sana kuliko Yanga? Wao walifungwa na Ihefu hivi karibuni kwani walihongwa? Yanga ina unyonge gani wa kushindwa kuifunga Prisons?" Alihoji Bumbuli.

Alisema hawatokubali kulinyamazia jambo hili kwa sababu maana ya mchezaji huyo ni kutaka kuiharibu nembo ya klabu na kuonekana kuwa timu yao haiwezi kuwafunga mpaka watoe kitu fulani.

Habari Kubwa