Yanga kwenda Mauritius kesho na ndege ya kukod

11Feb 2016
Somoe Ng'itu
Dar es Salaam
Nipashe
Yanga kwenda Mauritius kesho na ndege ya kukod

PESA inaongea, wawakilishi wa Tanzania Bara katika mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga sasa wataondoka nchini kesho kuelekea Mauritius kwa ajili ya mechi yao ya kwanza ya michuani hiyo itakayofanyika Jumamosi dhidi ya wenyeji Cercle de Joachim imeelezwa.

Awali Kocha Mkuu wa Yanga, Hans van der Pluimj alisema kuwa kikosi chake kingeondoka nchini jana kwenda Mauritius na kutoa nafasi kwa wachezaji wake kuzoea hali ya hewa na baadaye kuendelea na kambi ya muda huko ili kujinoa kuwakabili mahasimu wao Simba.

Akizungumza na gazeti hili, Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh, alisema kwamba sababu ya kuahirisha safari yao jana ilitokana na kukosa ndege ya moja kwa moja na kuambiwa kwamba wangesubiri kuunganisha ndege kwa zaidi ya saa tano mjini Johanesburg, Afrika Kusini.

Meneja huyo alisema kwamba, baada ya viongozi kupata taarifa hizo, benchi la ufundi lilishauri kuachana na usafiri huo na kusaka mwingine ambao hautawachosha wachezaji wao.

"Safari itakuwa sasa ni Ijumaa, kama tungesafiri leo (jana) tungelazimika kukaa muda mrefu kule Afrika Kusini kusubiri ndege nyingine ya kuunganisha jambo ambalo lingewachosha wachezaji wetu, lakini hiyo Ijumaa utaratibu unaandaliwa wa kuondoka na ndege ya moja kwa moja kutoka Dar mpaka Mauritius," alisema meneja huyo.

Aliongeza kuwa kama timu ingeondoka jana alfajiri, wangelazimika kukaa kwenye Uwanja wa Ndege kule Afrika Kusini kuanzia saa mbili na nusu asubuhi hadi saa nane mchana.

Kutokana na mabadiliko hayo, sasa Yanga jana jioni ilitarajia kuendelea na mazoezi yake kwenye Uwanja wa Polisi Kurasini na leo pia itafanya mazoezi ya mwisho kabla ya kuanza safari.

Inadaiwa kuwa usafiri huo watakaoondoka nao kesho utakuwa ni wa kukodi na utaisubiri timu kurejea nayo nchini baada ya kumaliza mchezo wao unaotarajiwa kufanyika kuanzia saa 9:30 mchana kwa saa za Tanzania.

Wachezaji 23 wanaotarajiwa kuondoka kesho ni pamoja na makipa; Ally Mustafa
‘Barthez’ na Deogratius Munishi 'Dida' wakati mabeki ni Juma Abdul, Mbuyu
Twite , Oscar Joshua, Mwinyi Hajji Mngwali, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kelvin
Yondani, Vincent Bossou, Pato Ngonyani wakati viungo ni Said Juma ‘Makapu’, Salum Telela, Thabani Kamusoko, Haruna Niyonzima, Simon Msuva, Issoufou Boubacar na Deus Kaseke.

Safu ya ushambuliaji itawakilishwa na Malimi Busungu, Paul Nonga, Amissi
Tambwe na Donald Ngoma wakati viongozi wa benchi la Ufundi wataongozwa na
Kocha Mkuu; Hans van der Pluijm, Kocha Msaidizi, Juma Mwambusi, Kocha wa Makipa, Juma Pondamali, Nassor Matuzya (Daktari), Hafidh (meneja), Mchua Misuli; Jacob Onyango na Mtunza Vifaa, Mohammed Mpogolo.

Habari Kubwa