Yanga : Lipuli itakufa hivi

15Mar 2019
Faustine Feliciane
Dar es Salaam
Nipashe
Yanga : Lipuli itakufa hivi
  • ***Hata hivyo itashuka Samora bila ya Ajibu, Dante na Ninja ambao...

VINARA wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga walitua salama mkoani Iringa jana jioni tayari kuwakabili wenyeji Lipuli Fc katika mchezo wa ligi hiyo utakaochezwa kesho lakini ikiwa bila ya nyota wake watatu wa kikosi cha kwanza.

Nyota ambao itawakosa katika mchezo huo na wamebaki jijini Dar es Salaam ni pamoja na Ibrahim Ajibu, Andrew Vincent ‘Dante’ na Abdallah Shaibu ‘Ninja' kutokana na sababu tofauti.

Kukosekana kwa nyota hao hasa wachezaji wa safu ya ulinzi ya Yanga kupwaya na kuwapa Lipuli FC nafasi ya kuondoka na pointi zote tatu kama washambuliaji wake watatumia vema nafasi watakazotengeneza.

Mratibu wa timu hiyo, Hafidh Saleh aliiambia Nipashe kutoka Iringa kuwa nahodha wao, Ajibu ameshindwa kusafiri na timu kutokana maumivu ya nyonga huku Ninja akiwa na adhabu ya kufungiwa kucheza mechi tatu.

“Dante ni majeruhi pia, hatukuweza kusafiri naye, Ajibu yeye alikuwa akilalamika maumivu ya nyonga hivyo hatoweza kucheza,” alisema Saleh.

Naye Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Noel Mwandila, alisema licha ya kukosekana kwa wachezaji hao bado watapambana kuhakikisha wanapata matokeo mazuri kwa sababu wachezaji wengine waliobakia wana uwezo kutekeleza majukumu watakayopewa.

“Hatuwezi kusema hiyo itakuwa sababu ya sisi kutofanya vizuri, nawaamini wachezaji wote tuliokuja nao huku na kila mmoja atafanya kazi yake kuhakikisha tunatimiza tulichokikusudia, malengo yetu ni ushindi,” alisema Mwandila.

Liongeza kuwa wanawaheshimu Lipuli lakini wasitegemee wepesi kwa sababu tya kukosekana kwa nyota hao.

Mwandila ataiongoza timu hiyo kutokana na Kocha Mkuu, Mwinyi Zahera kurejea kwao Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ili kutekeleza majukumu yake ya Timu ya Taifa ya nchi ambayo yeye ni Kocha Msaidizi.

Yanga yenye pointi 64 inaongoza ligi hiyo yenye timu 20 wakati Lipuli wenyewe wako katika nafasi ya tano katika msimamo baada ya kujikusanyia pointi 41 baada ya kucheza mechi 30.

Habari Kubwa