Yanga majaribuni Mwanza

25Oct 2020
Somoe Ng'itu
Mwanza
Nipashe Jumapili
Yanga majaribuni Mwanza
  • ***Ni katika vita nyingine ya kuwania pointi tatu muhimu za Ligi Kuu Bara dhidi ya KMC...

VITA ya kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara inatarajia kuendelea kwa wenyeji KMC FC kutoka Dar es Salaam kuwakaribisha Yanga kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini, Mwanza.

Akizungumza na gazeti hili jana, Kocha Mkuu wa Yanga, Cedric Kaze, alisema kikosi chake kiko tayari kwa mchezo huo na wamejipanga kuongeza umakini kutokana na rekodi nzuri na wapinzani wao msimu huu.

Kaze alisema bado anaendelea kukijenga vyema kikosi chake, hivyo baadhi ya idara zinaendelea kuimarika taratibu, lakini wataingia uwanjani wakiwa na malengo ya kusaka ushindi na si matokeo mengine.

Mrundi huyo alisema anafurahi kuona ushindani wa namba na juhudi zinazoonyeshwa na wachezaji wa timu hiyo ambao pia wanahitaji kufanya vizuri katika kila mechi watakayocheza.

"Katika soka hakuna mechi rahisi, hakuna mechi nyepesi, ila mechi zote ni muhimu, tumejiandaa kupata matokeo mazuri, pointi tatu ni muhimu huku kikosi kikiendelea kuonyesha ubora," alisema Kaze.

Kocha huyo aliwataka mashabiki na wanachama wa timu hiyo kuendelea kuimarisha umoja ili kuwaongezea nguvu wachezaji wao ambao wanaingia uwanjani kupambana.

"Asante Yanga, tulianza vizuri na ninatumaini Jumapili tutakuwa pamoja, tumejipanga na tunategemea ushindi," Kaze aliongeza.

Kocha wa KMC, Habib Kondo, maandalizi kuelekea mchezo wa leo yamefanyika vizuri na walifika jijini Mwanza mapema ili kujiweka tayari kuikabili Yanga.

Kondo alisema wamekwenda Mwanza kwa sababu moja tu ya kusaka ushindi lakini watashuka uwanjani wakiwa wanawaheshimu wapinzani wao.

"Tuna siku tatu hapa Mwanza, tumekamilisha maandalizi yetu  leo( jana)kuelekea mchezo huo, tuko tayari kwa ajili ya kupambana ili kupata pointi, tunaufikiria zaidi mchezo huu na michezo iliyopita haiko katika mipango yetu," alisema Kondo.

Kocha huyo aliongeza kila mechi ina mikakati yake, hivyo wameshasahu matokeo  ya mechi zilizopita na sasa wanaiangalia Yanga ambayo hawaihofii.

"Michezo iliyopita imeshapita, wao walicheza na Polisi Tanzania na sisi tulicheza mechi yetu, japokuwa Yanga ni timu kubwa, timu

Alisema hana mchezaji ambaye ni majeruhi na kila nyota aliyeko Mwanza yuko tayari kupambana kuondoka na ushindi.

"Tumekuja Mwanza kusaka pointi tisa katika mechi zetu tatu, tunaanza na Yanga, halafu tunaenda kuchukua kwa Gwambina na Biashara, baada ya hapo tutarejea Dar es Salaam na tutarudi kwa kishindi kutokana na ushindi ambao tutakuwa tumepata kwenye mechi hizo," Kondo alisema.

Wakati huo huo, katika mechi ya mapema jana mchana, Ihefu FC ilipata sare ya bila kufungana na Namungo FC katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Sokoine jijini, Mbeya.

Habari Kubwa