Yanga: Mbao daraja la Pyramids Kirumba

22Oct 2019
Somoe Ng'itu
Dar es Salaam
Nipashe
Yanga: Mbao daraja la Pyramids Kirumba
  • ***Zahera asema morali wa mechi hiyo ya Caf itapatikana leo wakishuka dimbani huku akiwataka...

SAFARI ya kuwania ufalme wa Ligi Kuu Tanzania Bara inatarajia kuendelea kwa wawakilishi pekee wa nchi waliobaki kwenye mashindano ya kimataifa, Yanga kukutana na wenyeji wao, Mbao FC katika mechi ya ligi hiyo itakayochezwa leo kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera, picha mtandao

Akizungumza na gazeti hili jana, Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera, alisema wachezaji wake wako imara na tayari kwa mchezo huo ambao wanahitaji kupata ushindi ili kuongeza morali kuelekea mechi yao ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Pyramids kutoka Misri.

Zahera, kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), alisema kila mchezaji anafahamu umuhimu wa mechi hiyo na wamejiandaa kwenda kupambana ili malengo yao ya kuondoka na pointi tatu yaweze kutimia.

"Tumejiandaa na tumejipanga vizuri, mechi itakuwa nzuri na itakuwa na ushindani, wao wanaijua Yanga, na sisi tunawajua, tutapambana ili kupata matokeo mazuri, nimewaambia kikubwa akili zao, ziwe katika mechi hii ya kesho (leo), na si mechi zilizopita," alisema Zahera.

Alisema kikosi chake kimekamilika, baada ya wachezaji wote waliokuwa kwenye timu ya Taifa (Taifa Stars), kuungana na wenzao ili kujinoa kuwakabili wenyeji wao.

Naye Mratibu wa timu hiyo, Hafidh Saleh, alisema hali ya hewa ya Mwanza ni nzuri na jana asubuhi kikosi chao kilifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Nyamagana wakati jioni kilijifua kwenye Uwanja wa CCM Kirumba.

Aliwataja wachezaji watakaokosekana katika mchezo huo kuwa ni pamoja na Juma Mahadhi, Issa Bigirimana, Cleofas Sospeter na Mohammed Banka.

Yanga ambayo mechi yake ya mwisho ilipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Coastal Union, ina pointi nne na imecheza michezo mitatu wakati Mbao FC yenye pointi tano, imeshuka dimbani mara tano.

Ligi hiyo inayotoa mwakilishi wa Tanzania Bara katika mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika, inatarajia kuendelea tena kesho kwa vinara, Simba ambao pia ni mabingwa watetezi kuvaana na Azam FC kwenye Uwanja wa Taifa jijini.

Habari Kubwa