Yanga: 'Mchawi' wa ushindi ugenini huyu

28Feb 2019
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Yanga: 'Mchawi' wa ushindi ugenini huyu
  • ***Yaifuata Alliance kwa tahadhari, huku ikizitaja Simba, Azam kama...

KIKOSI cha Yanga kinatarajia kuondoka jijini Dar es Salaam leo, kwenda mjini Mwanza kucheza dhidi ya Alliance Jumamosi kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara inayoendelea nchini kwa tahadhari kubwa baada ya kubaini sababu ya kupata tabu kuibuka na ushindi inapocheza ...

ugenini.

Tangu msimu huu wa Ligi Kuu uanze, Yanga imepoteza mechi mbili tu na kutoka sare nne.

Katika mechi ilizopoteza, moja ni Uwanja wa Taifa dhidi ya Simba na nyingine ugenini katika dimba la Kambarage Shinyanga dhidi ya Stand United zote ikikubali kipigo cha bao 1-0.

Mechi ilizotoka sare ni dhidi ya Simba ya bila kufungana katika mzunguko wa kwanza, matokeo kama hayo ikiyapata pia dhidi ya Singida United Uwanja wa Namfua.

Wakati sare ya bao 1-1 ikiwa ni katika mzunguko wa kwanza dhidi ya Ndanda FC Uwanja wa Taifa na kisha dhidi ya Coastal Union raundi ya pili kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.

Hata hivyo, akizungumza na Nipashe jana, Mratibu wa Yanga, Hafidh Salehe, alisema kikosi kinaondoka leo kwa ndege kuelekea Mwanza kwa ajili ya mechi hiyo, ambayo amesema kuwa inatarajiwa kuwa kali na ya kusisimua kutokana na ubora walionao Yanga kwa sasa, lakini pia Alliance inapokuwa nyumbani, ambayo kwenye mzunguko wa pili imeonekana kuimarika.

Akifafanua ugumu wa kuibuka na ushindi kwa Yanga hata kwa Simba, alisema hakuna kitu kingine zaidi ya timu hizo kuzikamia hususan zinapokuwa kwao tofauti na zinapocheza na timu nyingine kwenye ligi hiyo.

"Alliance ni timu nzuri na hasa kwenye kipindi hiki cha karibuni, lakini sisi tunakwenda kucheza kama mechi zingine zote kwa sababu hizi timu za mikoani zote zinapocheza na Yanga na Simba zinacheza kwa kupania sana, hili sisi tunalijua na tumejipanga kwa hilo," alisema.

Alisema Yanga haina majeruhi wa kutisha, hivyo Kocha Mkuu Mwinyi Zahera, atakuwa na wigo mpana wa kuchagua kikosi anachotaka kukianzisha.

"Hatuna majeruhi wa kutisha wala kadi, kwa hiyo wachezaji wote wako vizuri ni juu tu ya mwalimu," alisema.

Akizungumzia mbio za ubingwa, licha ya timu yao kuwa kileleni mwa ligi hiyo, mratibu huyo alisema mpaka ligi ilipofikia, ni timu tatu tu ndizo zinazoonekana moja inaweza kubeba taji hilo.

"Timu yoyote ile kati ya sisi [Yanga), Simba na hata Azam, bado huwezi kumwondoa kwenye mbio hizo, lakini sisi kama Yanga tumejipanga kuhakikisha tunauchukua," alisema.

Mbali na kuifunga Namungo FC bao 1-0 kwenye mechi ya Kombe la FA, Yanga ilitoka kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mara ya mwisho na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mbao FC kwa mara ya kwanza, baada ya misimu miwili Februari 20, hivyo Jumamosi watawavaa 'wauza mbao' hao kwa kujiamini.

Timu hiyo inaongoza ligi ikiwa na pointi 61 na michezo 25 iliyocheza, lakini ikiwa kwenye presha kali kutokana na mahasimu wao wa jadi, Simba kushinda mechi nne mfululizo na kuonekana kupunguza wigo wa pointi.

Alliance, ambayo kwenye mzunguko wa kwanza ilikuwa inashikilia mkia, iko kwenye nafasi ya saba ikiwa na pointi 36 kwa michezo 28 iliyocheza.

Habari Kubwa