Yanga mwendo mdundo Ligi Kuu

26Oct 2020
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Yanga mwendo mdundo Ligi Kuu
  • ***Yazidi kuikimbiza Azam FC, Waziri Junior akitangaza ufalme Kirumba kwa kuitungua KMC huku...

WAZIRI Junior jana alifunga bao lake la kwanza kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu akiwa na klabu yake mpya ya Yanga kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza, akiifanya kutembea 'mwendo mdundo' kwa kuondoka na pointi zote tatu wakati ikishinda mabao 2-1 dhidi ya KMC FC.

Waziri ambaye alijiunga na Yanga akitoka Mbao FC, alifunga bao hilo kwa kichwa, akiunganisha kona iliyochongwa na Farid Mussa dakika ya 61 ya mchezo kwenye mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara na baada ya kufunga alionyesha fulana yake ya ndani iliyoandikwa "The King of CCM Kirumba" (Mfalme wa CCM Kirumba), hiyo ikitokana na msimu uliopita wakati akiichezea Mbao FC kufunga mabao mengi wakati wakiutumia uwanja huo.

Kwenye mechi hiyo, Yanga ilishtukizwa kwa kufungwa bao dakika ya 26 likifungwa na Hassan Kabunda kwa shuti kali nje ya 18.

Mfungaji alipata pasi ndefu kutoka kwa Israel Patrick na kuwahadaa mabeki wa Yanga, kabla ya kuachia shuti kali lililomshinda kipa Metacha Mnata na kujaa wavuni.

Kabla ya bao hilo, KMC ilianza kulitia msukosuko lango la Yanga dakika ya 15, lakini shuti la Kenny Ally lilitoka nje kidogo ya lango.

Yanga ilijibu dakika ya 22 wakati krosi ya Kibwana Shomari nusura izae bao, lakini mastraika wa Yanga, Waziri na Michel Sarpong wote waliruka juu na kupiga hewa badala ya mpira, ambao ukatoka nje.

Dakika mbili baadaye shuti la Sarpong lililokuwa kilielekea golini lilimgonga mchezaji mwenzake wa Yanga na kurejea uwanjani, sekunde chache kabla ya shuti la Deusa Kaseke kutoka nje la lango.

Kabunda aliipatia KMC bao la kuongoza dakika ya 26, baada ya kupata pasi ndefu kutoka kwa Israel Patrick na kuwahadaa mabeki wa Yanga, kabla ya kuachia shuti kali lililomshinda kipa Metacha na kujaa wavuni.

Feisal Salum, nusura aifungie Yanga bao, baada ya kombora lake kali kugonga mlingoti wa juu na kurejea uwanjani dakika ya 38.

Yanga ilisawazisha bao lake kwa njia ya penalti, baada ya Sarpong kumuhadaa mwamuzi kwa kujiangusha akiwa ndani ya eneo la hatari na Tuisila Kisinda akaijaza wavuni, akimzidi ujanja Juma Kaseja anayesifika kwa kuokota penalti.

Hii ni mara ya pili kwa Kaseja msimu huu kupigiwa penalti, kwani kwenye mechi kati ya timu yake na Coastal Union, aliokoa penalti iliyopigwa na Yusuph Soka mechi ambayo aliisaidia timu yake kutoka sare ya bao 1-1.

Kipindi cha pili, hakukuwa na kosakosa nyingi, badala yake timu zote zilionekana kucheza kwa wasiwasi zaidi na kushindwa kutengeneza nafasi.

Kwa matokeo hayo, Yanga bado imeendelea kung'ang'ania kwenye nafasi ya pili, ikifikisha pointi 19 nyuma ya vinara Azam FC ambao leo wanashuka kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro kucheza dhidi ya Mtibwa Sugar ikiwa na pointi 21, zote zikiwa zimecheza mechi saba.

KMC inabakia na pointi zake 11, ikiwa imecheza mechi nane.

Katika mechi zingine zilizopigwa jana Polisi Tanzania ilikubali kipigo cha 1-0 kutoka kwa Biashara Mara United katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha wakati Mwadui FC ikilala kwa mabao 6-1 dhidi ya JKT Tanzania.

Habari Kubwa