Yanga na siri za Gor Mahia

14Jun 2018
Faustine Feliciane
DAR ES SALAAM
Nipashe
Yanga na siri za Gor Mahia

IKIWA umebaki mwezi mmoja kabla ya kuumana na mabingwa wa Kenya, Gor Mahia, Yanga imeanza mikakati ya chini kwa chini kuhakikisha inaibuka na ushindi wake wa kwanza kwenye kundi lao la michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Gor Mahia.

Yanga itaumana na Gor Mahia Julai 18, mwaka huu kwenye Uwanja wa Moi Kasarani nchini Kenya.

Kocha msaidizi wa timu hiyo, Noel Mwandila, aliliambia Nipashe kuwa mchezo huo hautakuwa rahisi na kwa kuwa wanahitaji ushindi mikakati wanaianza mapema.

Alisema wameiona Gor Mahia kwenye michuano ya SportPesa iliyomalizika hivi karibuni nchini Kenya na kugundua ni timu nzuri na wao (Yanga), lazima wajipange.

"Tutaanza mikakati mapema kuhakikisha mchezo huo tunashinda, Gor ni timu imara tumeiona, lakini kwa muda tulionao naamini tutakuwa sawa kuwakabili," alisema Mwandila kabla ya kuondoka kwenda mapumzikoni nchini kwao.

Yanga inahitaji ushindi kwenye mchezo huo ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kushika nafasi mbili za juu zitakazoifanya kusonga mbele kwa kuwa imevuna pointi moja pekee kwenye michezo miwili iliyocheza.

Yanga ilianza michuano hiyo kwa kipigo cha mabao 4-0 kutoka USM Alger ugenini kabla ya kubanwa nyumbani na kulazimishwa suluhu dhidi ya Rayon Sports ya Rwanda.

Kikosi hicho cha Yanga kimepanga kuanza mazoezi Juni 25, mwaka huu ambapo imepangwa kuwa siku ya wachezaji na makocha kukutana na kuanza maandalizi.

Wachezaji wa kigeni wanatarajiwa kuwasili nchini kuanzia Juni 23 kuungana na wazawa kuanza mazoezi.

Habari Kubwa