Yanga, Ndanda hapatoshi Bara

08Nov 2019
Somoe Ng'itu
Dar es Salaam
Nipashe
Yanga, Ndanda hapatoshi Bara

IKIWA chini ya kocha mpya wa muda, Boniface Mkwasa "Master", Yanga inatarajia kuteremka ugenini kuwakabili Ndanda FC katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara itakayochezwa leo kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona, ulioko mkoani Mtwara.

Kuelekea mchezo huo, Mkwasa, alisema kuwa wanatarajia mchezo huo utakuwa mgumu na wenye ushindani kutokana na wapinzani wao kuwapa changamoto kila wanapokutana.

Mkwasa alisema kuwa anaamini wachezaji wake watakuwa makini kuhakikisha wanapata matokeo mazuri katika mchezo huo, ambao kwa Yanga ni wa tano, tangu kuanza kwa msimu huu.

Alisema kuwa katika mechi hiyo, atawakosa wachezaji wake nane ambao ni pamoja na Juma Balinya, Lamine Moro, Abdul-Aziz Makame, Ali Ali, Maybin Kalengo, Paul Godfrey, Cleofas Sospeter na Feisal Salum "Fei Toto".

Mechi nyingine za ligi hiyo zinazotarajiwa kuchezwa leo ni kati ya Azam FC dhidi ya Biashara United kwenye Uwanja wa Azam Complex wakati KMC FC yenyewe itawakaribisha Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Uhuru jijini.

Habari Kubwa