Yanga: Ni vichapo tu

09Dec 2018
Somoe Ng'itu
DAR ES SALAAM
Nipashe Jumapili
Yanga: Ni vichapo tu
  • *** Zahera awaita mashabiki kushuhudia wakiipoteza Biashara Taifa leo kwa...

USHINDI! Ndio kitu pekee ambacho Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera, amewaandaa wachezaji wake kukisaka wakati watakapoikaribisha Biashara United kutoka Musoma katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara itakayochezwa leo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera.

Yanga ikiwa na mechi moja mkononi ina pointi 38 katika nafasi ya pili nyuma ya Azam FC yenye pointi 39, huku mabingwa watetezi, Simba wenye pointi 27, wana mechi mbili za viporo wakiwa katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi hiyo.

Akizungumza na gazeti hili jana, Zahera, alisema wanahitaji kuendelea na kasi ya ushindi katika kila mechi wanayocheza na hiyo ndiyo njia pekee ya kutimiza malengo ambayo wamejiwekea msimu huu.

Zahera alisema anawakumbusha wachezaji wake kuongeza umakini wanapokuwa uwanjani kwa sababu hakuna timu inayokubali "kusindikiza" wengine katika ligi hiyo ya juu Tanzania Bara.

Alisema wachezaji wake hawatawadharau wapinzani wao kutokana na ugeni kwenye ligi na badala yake wataingia uwanjani kwa kazi moja tu ya kusaka pointi tatu.

"Lengo letu ni kushinda kila mechi tunayocheza, kila timu iliyoko mbele yetu ni sawa na adui, tunachokiangalia ni kuendeleza kasi ya ushindi," alisema Zahera ambaye ameibuka Kocha Bora wa Novemba.

Alisema hawataangalia nafasi ya Biashara United katika msimamo wa ligi na badala yake wamejipanga kupambana nao kama walivyofanya katika mechi zilizotangulia.

Naye Kocha Msaidizi wa Biashara United, Madenge Omary, alisema wamejipanga kuwashangaza Yanga kwa kuwafunga na kuweka rekodi ya 'kuwatibulia'.

"Itakuwa mechi ngumu, Yanga hawajapoteza mechi hata moja, lakini sisi tunataka hii iwe mechi yetu ya pili kushinda msimu huu, hatutaki sare," alisema kocha huyo.

Mechi nyingine ya ligi hiyo inayotarajiwa kuchezwa leo ni kati ya Coastal Union dhidi ya Mbeya City itakayochezwa kuanzia saa 8:00 mchana kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.