YANGA NJE LIGI KUU

16Mar 2016
Somoe Ng'itu
Lete Raha
YANGA NJE LIGI KUU

NI kama wameondolewa kwa muda. Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara hawatacheza tena mechi nyingine yoyote mwezi huu.

Mara ya mwisho Yanga walicheza Ligi Kuu Machi 8, wakiwafunga 5-0 ndugu zao African Sports ya Tanga Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na watakuwa na mechi ya ligi hiyo tena Aprili 2, dhidi ya Kagera Sugar kwenye uwanja huo.

Na hiyo mechi ya Aprili 2 ipo shakani, kwani kama Yanga watafuzu hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika, watakuwa na mechi kati ya Aprili 8 na 10 dhidi ya Al AHly ya Misri, wakianzia nyumbani Uwanja wa Taifa kabla ya kurudiana kati ya Aprili 19 na 20.

Kwa kawaida Yanga hucheza mechi zake Jumamosi, maana yake mchezo wa kwanza na Ahly wanaweza kucheza Aprili 9 na kama wataamua kuomba muda wa maandalizi zaidi kabla ya mechi hiyo ngumu – maana yake mechi yao ya Ligi Kuu na Kagera inawezwa kuahirishwa pia.

Kiongozi mmoja wa Yanga ameiambia Lete raha jana kwamba hawawezi kurudia kosa la kucheza mechi katika wiki ya mchezo wao wa Ligi ya Mabingwa, kwani kabla ya kwenda kucheza na APR mechi ya kwanza ya Raundi ya Kwanza ya Ligi ya Mabingwa mjini Kigali, walicheza na African Sports mechi ya Ligi Kuu na matokeo yake, mshambuliaji wao tegemeo la mabao, Amissi Tambwe akaumia.

“Tambwe alishindwa kucheza Kigali kwa sababu aliumia kwenye mechi na Sports, tulifanya kosa ambalo hatuwezi kurudia.

Tunaomba TFF kama wanataka tufanye vizuri kwenye michuano hii, basi watupe muda wa kutosha wa maandalizi. Tunacheza ligi, ili tupate nafasi ya kucheza mashindano haya ya Afrika, sasa tunapopata nafasi hizi, lazima tuzitumie vizuri,”amesema.

Kwa mujibu wa marekebisho ya Ratiba ya Ligi Kuu yaliyotolewa jana, Azam FC watacheza na Stand United kesho Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam, wakati Simba SC watacheza na Coastal Union Jumamosi Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Bodi ya Ligi imelazimika kufanya marekebisho ya Ratiba ya Ligi Kuu kupisha ratiba ya timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars katika mechi za kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika 2017.

Taifa Stars itakuwa na mchezo wa kufuzu AFCON Kundi G dhidi ya Chad mjini N’Djamena Machi 23, kabla ya timu hizo kurudiana Machi 28, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Na baada ya mechi za mwishoni mwa wiki za michuano ya klabu barani, Afrika kundi la kwanza la wachezaji wa Stars linatarajiwa kuondoka Jumapili kuelekea Chad.

Yanga SC baada ya ushindi wa 2-1 kwenye mchezo wa kwanza wa Raundi ya Kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya APR Jumamosi mjini Kigali, watarudiana na timu hiyo ya jeshi la Rwanda Jumamosi wiki hii Uwanja wa Taifa.

Na Azam FC baada ya kushinda 3-0 mjini Johannesburg, Afrika Kusini dhidi ya wenyeji Bidvest Wits katika mchezo wa kwanza wa Raundi ya Kwanza Kombe la Shirikisho Afrika, watarudiana na timu hiyo Jumapili, Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Habari Kubwa