Yanga, Prisons ni ushindi na kisasi

15Feb 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Yanga, Prisons ni ushindi na kisasi

USHINDI na kisasi! Ndiyo unavyoweza kusema kutokana na kauli za kocha wa Yanga, Luc Eymael na wa Tanzania Prisons, Adolf Rishard, kuelekea mechi yao ya Ligi Kuu katika Uwanja wa Taifa leo.

Hiyo ni kutokana na wakati Eymael akisema kuwa hakuna namna leo ni ushindi tu, Rishard yeye amesema wanataka kuibuka na ushindi ili kulipa kisasi cha mzunguko wa kwanza.

Katika mchezo wa raundi ya kwanza timu hizo zilipokutana msimu huu kwenye Uwanja wa Samora mjini Iringa, Yanga ilishinda kwa bao 1-0 lililofungwa na Patrick Sibomana wakati huo ikiwa chini ya Boniface Mkwasa, kwa sasa kocha msaidizi.

Eymael aliliambia Nipashe: "Kwetu sisi mechi zetu ni ngumu na ushindani ni mkubwa matumaini yetu ni kuona tunashinda ili kuongeza nguvu ya kufika kwenye malengo yetu tuliyojiwekea, hatuna chaguo lingine zaidi ya kutafuta ushindi."

Naye kocha wa Prison, Rishard alisema: "Tunawaheshimu Yanga, tunaingia kwa umakini mkubwa kusaka pointi tatu na kulipa kisasi kutokana na mchezo wa kwanza tulipoteza."

Timu hizo zinakutana leo zote kila moja ikiwa na kumbukumbu yake, ambapo Yanga ilazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Mbeya City huku Prison ikikubali kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa wapinzani hao wa Yanga katika uwanja wa Jamhuri, Dodoma.

Baada ya mchezo huo Prison ilitakiwa kucheza dhidi ya Ruvu Shooting, lakini mchezo huo ukaahirishwa kutokana na uwanja kutokuwa na gari la kubebea wagonjwa (ambulance) kama kanuni zinavyoagiza.

Habari Kubwa