Yanga: Sababu kipigo Simba hii

14Jul 2020
WAANDISHI WETU
Dar es Salaam
Nipashe
Yanga: Sababu kipigo Simba hii
  • Eymael asema subirini msimu ujao, ageukia pointi 12 huku wachezaji na uongozi wakiomba radhi...

Kocha Mkuu wa Yanga, Mbelgiji Luc Eymael, amesema alijua mchezo wao dhidi ya Simba kwenye Kombe la FA juzi utakuwa mgumu, lakini hakutarajia timu yake kuchapwa 4-1, huku akieleza moja ya sababu iliyochangia kipigo hicho ni kutokana na baadhi ya wachezaji wake kutokuwa fiti kwa asilimia mia.

Akizungumza na gazeti hili, Eymael alisema nyota wake, Nahodha Papy Kabamba Tshishimbi na Haruna Niyomzima hawakuwa kwenye ubora wao kwa kuwa wametoka kwenye chumba cha majeruhi.

"Lakini baadhi ya wachezaji wangu hawakufuata maelekezo yangu, nilitegemea mchezo mgumu, lakini mabao tuliyofungwa yalikuwa mengi na hatukucheza kwenye ubora wetu," alisema Eymael.

Aidha, alisema kuwa Simba walikuwa bora zaidi eneo la katikati na hata safu yao ya ushambuliaji ilikuwa kwenye ubora na kuwapa kazi kubwa mabeki wake.

"Makosa yanatokeo kwenye mpira na unapokutana na timu bora inakuadhibu kutokana na makosa yako, kwa sasa tutapambana kuhakikisha tunamaliza vizuri michezo iliyobaki ya Ligi Kuu," alisema Eymael huku akiahidi kutengeneza timu ya ushindani msimu ujao.

Eymael alisema hakufurahishwa na kiwango cha wachezaji wake walichocheza katika mchezo huo, lakini akiwataka sasa kuweka nguvu katika michezo iliyobaki ya ligi ili kushika nafasi ya pili ambayo kwa sasa inashikiliwa na Azam FC.

Alisema baada ya kukosa nafasi ya kuiwakilisha nchi katika michuano ya kimataifa wanafanyia kazi mapungufu yao kwa ajili ya kuwania nafasi ya pili ambayo itakuwa ya heshima kwao.

“Simba walituzidi na kutumia makosa yetu kutufunga, pia  sijafurahishwa na matokeo pamoja na jinsi wachezaji wangu walivyocheza kwa kiwango cha chini, sasa nimewataka kuhakikisha tunafanya vizuri katika michezo minne iliyobaki,” alisema Eymael.

Kwa upande wa beki wa timu hiyo, Lamine Moro amekiri timu yao kuzidiwa katika mchezo huo dhidi ya Simba kwa kutumia makosa yao kupata ushindi mkubwa.

“Tumepokea matokeo, mchezo wa soka una matokeo ya kufungwa, kushinda na hata sare, wenzetu walitumia mapungufu yetu, sasa tunaendelea na mapambano katika michezo iliyobaki kutafuta alama muhimu ili tumalize ligi katika nafasi ya pili,” alisema beki huyo.

Katika hatua nyingine wachezaji na uongozi wa klabu ya Yanga umewaomba radhi wanachama na mashabiki wa klabu hiyo kutokana na kipigo hicho cha juzi.

Naodha msaidizi wa klabu hiyo, Juma Abdul, alisema matokeo waliyoyapata yamewaumiza sana na yametokana na makosa yao wachezaji uwanjani.

"Kwa niaba ya wachezaji wenzangu, nawaomba radhi wanachama na mashabiki wa klabu yetu kutokana na matokeo haya, ni kweli yanaumiza na hatukupaswa kuyapata," alisema Abdul.

Wakati Abdul akisema hivyo, Kaimu Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Simon Patrick, aliungana na nahodha huyo kuwaomba radhi mashabiki na kuwataka kuendelea kushikamana mpaka msimu utakapomalizika.

"Tumeona mapungufu ya kikosi chetu, tuendelee kushikamana kama klabu na haya yote yatafanyiwa kazi mwishoni mwa msimu huu ili msimu ujao tuwe na kikosi imara kitakachotupa furaha, uongozi unawaomba radhi mashabiki na wanachama wetu kwa matokeo haya," alisema.

Yanga imebakiza michezo minne ambapo kesho itaikaribisha Singida United ambayo tayari imeshashuka daraja, Julai 18 itaialika Mwadui FC, kabla ya kuifuata Mtibwa Sugar na kisha kufunga msimu ugenini dhidi ya Lipuli FC.

Habari Kubwa