Yanga sasa ya historia

17Jun 2019
Somoe Ng'itu
Dar es Salaam
Nipashe
Yanga sasa ya historia
  • ***Mwakalebela aeleza 'Kubwa Kuliko' ilivyoleta matumaini, mamilioni yamiminika usajili mastaa...

UONGOZI wa Yanga umesema klabu yao itaandika historia ya kufanya vema katika kila mashindano watakayoshiriki msimu ujao kutokana na mafanikio yaliyopatikana katika harambee yao maarufu "Kubwa Kuliko" iliyofanyika juzi kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, walikuwa wageni walioalikwa katika harambee hiyo ambayo ilikusanya ahadi na fedha taslimu kiasi cha Sh. milioni 920.

Akizungumza na gazeti hili jana, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela, alisema baada ya kufanikiwa kupata fedha hizo, wanaamini wataanza msimu mpya kwa kishindo na watatimiza malengo yote waliyojiwekea.

Mwakalebela alisema wamejipanga kurejesha heshima na hadhi ya Yanga ambayo wanachama wake wameikosa kwa kipindi cha misimu miwili mfululizo.

Alisema mafanikio yaliyoonekana katika harambee yao, umoja na ushirikiano kutoka kwa makundi yote ya wanachama, ni vitu vinavyowapa nguvu viongozi kwamba hakuna kitakachokwama.

"Tumejipanga kuweka historia, si katika Ligi Kuu Tanzania Bara tu, kila mashindano tutakayoweka mguu, Yanga ile mliyokuwa mnaijua ndiyo itarudi, kila kitu kitakwenda vizuri, tutashindana na tutashinda," alisema Mwakalebela.

Aliongeza kuwa kutokana na fedha walizopata, kikosi chao kitaendelea kujiimarisha kwa kusajili wachezaji wenye uzoefu na kuwalipa malimbikizo ya mishahara baadhi ya nyota wao wa zamani ambao wanadai.

"Tumefanikiwa kwa kiwango kikubwa, malengo yametimia, tunasema asanteni Wanayanga wote, hii ni timu yetu, lazima tushiriki kuisaidia kwa kila hali, sisi ni mashahidi, tukutane uwanjani," Mwakalebela alisema.

Waziri Mkuu, Majaliwa katika hotuba yake hapo juzi alisema kama hakuna Yanga imara, basi hakutakuwa na ushindani kwenye Ligi Kuu na mashindano mengine ya nje ambayo timu za hapa nchini zitashiriki.

"Naomba nimalizie, bila Yanga imara, huwezi kuwa na Simba imara, na bila Simba imara, huwezi kuwa na Yanga imara," Waziri Mkuu huyo ambaye pia ana taaluma ya ukocha wa mpira wa miguu mwenye leseni inayotambuliwa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf) alihitimisha.

Naye Rais Kikwete aliwataka viongozi wa Yanga kuhakikisha wanawekeza katika soka la vijana ili baadaye kuisaidia Timu ya Taifa (Taifa Stars), badala ya sasa kuwalipa fedha nyingi makocha ambao wanawaimarisha wachezaji wengi wa kigeni wanaokwenda kuzichezea nchi zao, inapofika suala la utaifa.

Rais Kikwete aliwataka pia mashabiki wa Yanga kuacha kuwa wanyonge wanapokwenda viwanjani na badala yake kujitokeza kwa wingi na kuishangilia timu yao kama wanavyofanya watani zao, Simba.

Habari Kubwa