Yanga sasa yabadili mfumo, Simba kiama

06Nov 2016
Faustine Feliciane
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Yanga sasa yabadili mfumo, Simba kiama
  • ***Wakati Omog akipanga kuzoa tena pointi Uhuru leo, Pluijm ataivaa Prisons kivingine baada ya kusoma makosa...

KIVUMBI cha Ligi Kuu Tanzania Bara kinaendelea tena leo, mabingwa watetezi, Yanga wakiwa na kibarua kigumu jijini Mbeya, wakati vinara wa ligi hiyo, Simba wakiwa Uwanja wa Uhuru wakiwania kuendeleza rekodi yao ya kutofungwa baada ya kucheza mechi13.

Yanga ambayo Jumatano ilikumbana na kipigo cha 2-1 mbele ya Mbeya City, leo itakutana na Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Sokoine huku kocha Hans van der Pluijm akipanga kubadilisha mfumo wa uchezaji kutoka pasi fupi fupi na kutumia pasi ndefu.

Akizungumza na Nipashe jana, Pluijm, alisema wana kila sababu ya kuhakikisha wanaondoka na pointi tatu kwenye mchezo wa leo na tayari amewapa wachezaji wake mbinu hiyo ya pasi ndefu ambayo anaamini itaiangamiza Prisons.

"Matokeo ya mchezo uliopita tumeyaondoa kichwani..., tutacheza soka letu la kasi na pia kutakuwa na mabadiliko kidogo ya kiufundi yote ikiwa ni kuhakikisha tunapata pointi tatu," alisema Pluijm.

Kwa upande wa kocha wa Prisons, Abdul Mingange, alisema pasipo kuangalia matokeo ya mechi zilizopita baina yao, bado mchezo wa leo ni mgumu na hautabiriki.

Wakati Yanga ikijaribu kusaka pointi tatu jijini Mbeya, katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, vinara Simba wenyewe watakuwa wageni wa African Lyon.

Kocha wa Simba, Mcameroon Joseph Omog, alisema mchezo huo wa leo wanauchukulia kwa uzito sawa na michezo mingine iliyopita.

"Lengo tunataka kuendeleza rekodi yetu ya ushindi, wachezaji wanalitambua hili na wataingia uwanjani kusaka pointi tatu," alisema Omog.

Simba inaendelea kuongoza ligi ikiwa na pointi 35 baada ya kucheza michezo 13 huku ikiizidi Yanga inayoshika nafasi ya pili kwa pointi nane. Azam ambayo nayo imecheza 13 inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 22 sawa na Stand United iliyoshuka dimbani mara 14.

Michezo mingine ya Ligi Kuu leo, Azam watakuwa ugenini kucheza na Mbao FC kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, JKT Ruvu yenyewe itaikaribisha Toto African, Kagera Sugar wakiwa kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba watawakaribisha Ruvu Shooting wakati Ndanda FC watakuwa wenyeji wa Stand United mkoani Mtwara.

Habari Kubwa