Yanga sasa yasubiri kupindua meza CAF

13Sep 2021
Na Waandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Yanga sasa yasubiri kupindua meza CAF

WAWAKILISHI wa Tanzania kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga ya Dar es Salaam na KMKM ya Zanzibar, jana walishindwa kuutumia vema uwanja wa nyumbani baada ya kuchapwa kukubali vipigo katika mechi zao za awali za Ligi ya Mabingwa Afrika, hivyo sasa kujipanga kwa ajili ya kwenda .....

kupindua matokeo 'meza' ugenini kwenye mechi za marudiano mwishoni mwa wiki.

Yanga ambayo iliwakaribisha wageni wao Rivers United ya Nigeria, ilikubali kipigo cha bao 1-0 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam wakati ndugu zao wa Zanzibar, KMKM wakiwa dimba la Amaan wakiangukia pua kwa mabao 2-0 dhidi ya Al-Ittihad ya Libya.

Kwa matokeo hayo, Yanga sasa inahitaji kupata ushindi kuanzia mabao 2-0 kwenye mechi ya marudiano wakati KMKM yenyewe ikihitaji kushinda kuanzia mabao 3-0 ili kutinga raundi ya kwanza ya michuano hiyo.

Bao lililopeleka simanzi kwa Yanga lilifungwa na Moses Omone dakika ya 51, mpira ukigushwa na wachezaji wawili, kabla ya kumfikia mfugaji aliyeukwamisha nyavuni kwa kichwa. Ilikuwa krosi ya Lookman Binuyo, iliyokwenda kwa Enyiama Kazie ambaye aliupiga kichwa, kabla ya mfungaji hajaumalizia wavuni.

Baada ya bao hilo, Yanga ilionekana kuzinduka kutoka usingizini, lakini mara nyingi pasi zao za mwisho zilikuwa hazifiki kwa walengwa, au wachezaji wao kuwa na papara wanapofika golini.

Yanga ilianza mechi kwa kasi, na iliwachukua sekundi 29 tu kulifikia lango la Rivers United, wakati Yacouba Songne alipoambaa na mpira kwenye wingi ya kushoto, kabla ya kuurudisha nyuma, ukamkuta Zawadi Mauya, akiwa mita zipatazo 30 kutoka langoni, akakandamiza shuti kali lililopita juu la lango.

Baada ya hapo, mpira ulichezwa zaidi katikati ya uwanja, na kwenye dakika ya 19, Yanga nusura iandike bao kwa mkwaju wa faulo uliopigwa kiufundi na Adeyum Selemani, lakini mpira uliparaza nyavu za juu, huku wengine wakidhani kuwa ni bao.

Dakika moja baadaye, Heritier Makambo, aliingia ndani ya eneo la hatari na kuachia shuti la mguu wa kushoto uliompita kipa wa Rivers United Sochima Elum. Wakati kila mmoja akitazamia mpira ukwame wavuni, ulitoka sentimeta chache kwenye lango.

Yacouba, kwa mara nyingine, aliikosesha Yanga bao dakika ya 30, kwa kumegewa pande kutoka kwa Feisal Salum, lakini shuti lake akiwa karibu na goli, lilitoka nje ya lango.

Wageni, ambao walikuwa wakifika golini kwa Yanga kwa kuvizia, hatimaye walilitia msukosuko lango la Yanga dakika ya 41, Moses akikosa bao la wazi akiwa na kipa Djigui Diarra, kabla ya kusawazisha makosa yake dakika ya 51 kipindi cha pili.

Yanga iliwatoa Makambo aliyeumia na nafasi yake ikachukuliwa na Yusuph Athumani, Yacouba alitoka na kuingia Ditrim Nchimbi, huku Zawadi Mauya naye akienda nje, Saido Ntibazonkiza akiingia.

KMKM na sababu ya kichapo

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mechi hiyo Kocha Msaidizi wa KMKM, Ali Vuai Shein, alisema kitendo cha kubadilishwa mchezo wao na kuchezwa jana badala ya juzi kilichangia kuwaondoa ari wachezaji wake, pia wachezaji wake wanne tegemeo walikutwa na maambukizo ya virusi vya corona hivyo kuwa pengo kubwa kwao. Mabao ya Al-Ittihad katika mechi hiyo yalifungwa na Muad Eisay dakika ya 45 na Rabia Alshadi dakika ya 84.

Habari Kubwa