Yanga SC: Kagere shida sana kwetu

27Sep 2018
Somoe Ng'itu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Yanga SC: Kagere shida sana kwetu
  • ***Bocco hatacheza na Okwi siku hizi hafungi, hivyo Simba itakuwa...

WAKATI kikosi cha Yanga kinajifua kwa saa zaidi ya tatu kwa siku ili kuhakikisha kinakuwa imara na kuweza kuibuka na ushindi katika mechi ya Jumapili dhidi ya Simba, uongozi wa timu hiyo unamhofia mshambuliaji wa mabingwa watetezi, Meddie Kagere.

Meddie Kagere..

 

Akizungumza na gazeti hili jana, Mratibu wa Yanga, Hafidh Saleh, alisema kuwa malengo ya kufanya mazoezi kwa muda mrefu ni kuwaimarisha wachezaji wao ili waweze kuumudu mchezo huo unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.

Saleh alisema Kocha Mkuu, Mwinyi Zahera, anahitaji kuona wachezaji wanakuwa na kasi inayofanana kuanzia kipindi cha kwanza hadi cha pili.

"Mwalimu anataka wachezaji wacheze kwa kasi ile ile, amesema ukikubali kushuka, unatoa nafasi kwa mpinzani kupanda, ni mechi ngumu na yenye ushindani, kikubwa ni kulinda kiwango kwa muda wote," alisema kiongozi huyo.

Aliongeza kuwa wanaamini timu ikiwa imara, watapata pointi tatu muhimu na kuwafurahisha mashabiki wao ambao msimu uliopita walivuliwa ubingwa.

Naye Ofisa Habari wa timu hiyo, Dismas Ten, alisema jana kuwa Yanga haina wasiwasi na mechi hiyo ya Jumapili kwa sababu wachezaji wao muhimu wote watakuwapo.

"Wachezaji wa Yanga wote watakuwapo, ninamaana ya Tambwe (Amissi), Makambo (Heritier), Ajibu (Ibrahim), Ngasa (Mrisho) na Kaseke (Deus)...kwa Simba Bocco (John) hayupo na anayeweza kufunga ni Kagere, Okwi hafungi siku hizi," alisema Ten.

Yanga imeweka kambi yake Morogoro wakati Simba ya Mbelgiji, Patrick Aussems imebaki jijini.

Habari Kubwa