Ofisa Habari wa klabu hiyo, Hassan Bumbuli amesema hayakuwa malengo yao kupata matokeo hayo, lakini ndivyo ilivyotokea na hiyo inaonyesha jinsi ligi ilivyo ngumu.
Jumatatu iliyopita, Yanga illazimishwa suluhu nyumbani dhidi ya Prisons, Uwanja wa Benjamin Mkapa, hali iliyozua taharuki kwa wanachama na mashabiki wao.
"Tunajua matokeo yametuathiri, lakini tunatakiwa tusonge mbele. Ni matokeo ambayo yametupa changamoto na siku zote changamoto ni kipimo cha maarifa ya binadamu, badala ya kulumbana, tunatakiwa tutafute maarifa mapya. Mbio za ubingwa zipo pale pale, tusianze kutoka kwenye reli, tunaongoza ligi na tunatakiwa kushinda tu na si kupiga ramli ya nani ashinde nani apoteze kama wenzetu," alisema Bumbuli.
Alisema kuwa tayari kikosi hicho kimesharejea kambini kujiandaa na mechi dhidi ya Dodoma Jijini itakayochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma saa 1:00 usiku.
"Tumerejea kambini, benchi la ufundi limeona makosa yaliyojitokeza, watahakikisha wanafanyia kazi ili yasijirudie tena kwenye mechi dhidi ya Dodoma Jiji," alisema Bumbuli.
Wanachama na mashabiki wa Yanga wamekuwa na sintofahamu baada ya timu yao kutoka suluhu mfululizo kwenye mechi za kuelekea kumaliza msimu wa ligi, huku ikiwa kwenye nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa.
Ilitoka suluhu bila kufungana dhidi ya Simba Aprili 30, matokeo kama hayo ikayapata Mei 4 dhidi ya Ruvu Shooting, kabla ya Jumatatu iliyopita, kukutana na matokeo hayo hayo dhidi ya Prisons.