Yanga: Tutacheza na Simba Julai 3

17Jun 2021
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Yanga: Tutacheza na Simba Julai 3

KLABU ya Yanga imesema itakwenda uwanjani kucheza mechi yao dhidi ya Simba iliyopangwa kupigwa Julai 3, mwaka huu, kama ilivyokubaliana na serikali, Shirikisho la Soka nchini (TFF) na Bodi ya Ligi.

Kaimu Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Haji Mfikirwa alisema hakuna sehemu yoyote ambayo klabu yao imetoa taarifa kuwa haitopeleka timu uwanjani kama inavyosemwa na baadhi ya watu ambao si viongozi.

Kaimu Katibu mkuu huyo alisema hayo kufuatia wazee wa klabu hiyo waliojinasibu kuwa ni Baraza la Wazee wa Yanga kufanya mkutano kwenye klabu hiyo na kudai kuwa timu haitokwenda kucheza mechi baina yao ya Simba.

"Walichokieleza ni maoni yao, lakini si msimamo rasmi wa klabu. Klabu ya Yanga ina utaratibu wake wa kutoka tamko au taarifa rasmi na anayetakiwa kufanya hivyo ni Mwenyekiti, Katibu Mkuu na Msemaji wa Klabu na si mtu mwingine yoyote," alisema Mfikiriwa.

Kuhusu kutumia klabu kuelezea jambo hilo, ikiwamo nembo za wadhamini, Kaimu Katibu Mkuu alisema kuwa wazee hao waliomba kuongea, na wao waliwakubalia kama wazee, lakini jambo walilokwenda kuongea, wakaongeza na mengine ambayo hayakuwamo.

Habari Kubwa