Yanga: Tutafanya maajabu

04Aug 2018
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Yanga: Tutafanya maajabu
  • ***Yatangaza rasmi kuvunja mkataba na kipa wake Mcameroon...

LICHA ya kuwakosa baadhi ya wachezaji wake nyota katika mazoezi huko Morogoro, kikosi cha Yanga kimejipanga kuwashangaza USM Alger kutoka Algeria katika mechi ya hatua ya makundi ya mashindano ya Kombe la Shirikisho itakayofanyika Agosti 19 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mratibu wa Yanga, Hafidh Saleh alisema kuwa kila mchezaji amekuwa akionyesha bidii na ushindani kwenye mazoezi yanayoendelea na benchi la ufundi linaamini kambi hiyo itawaimarisha.

Saleh alisema kuwa Yanga itaingia ikiwa imara na tofauti katika mechi ijayo ya michuano hiyo ya kimataifa inayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) pamoja na kuanza vyema msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara itakayoanza kurindima hivi karibuni.

"Sasa hivi wachezaji wameanza kurejea katika hali ya kawaida, ingawa bado upepo ndani ya klabu haujatulia kama inavyotakiwa, tunaamini kambi ya Morogoro itatufanya tuingie kucheza na Waarabu (USM Alger) tukiwa imara zaidi," alisema Saleh.

Aliwataja wachezaji Ibrahim Ajib, Ramadhan Kabwili na Papy Tshishimbi bado hawajaripoti kambini kutokana na sababu tofauti.

"Ajibu, Kabwili hawajafika bado, ila tumewasiliana na Tshishimbi na tunamtarajia jioni ya leo (jana) ataungana nasi, kama hakutakuwa na dharura yoyote hapa katikati,  kwa muda uliobakia tukiwa pamoja, wachezaji wataimarika na tunaweza kuwashangaza Waarabu," aliongeza mratibu huyo.

Wakati huo huo bila ya kusema sababu yoyote, Yanga imetangaza kuvunja mkataba na aliyekuwa kipa chaguo la kwanza, Youthe Rostand ambaye mkataba wake na klabu hiyo ulikuwa umebakia mwaka mmoja.

Rostand ambaye ni raia wa Cameroon, alitua Yanga akitokea African Lyon ya jijini ambayo msimu ujao itacheza tena Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kikosi cha Yanga kitacheza mechi ya kirafiki dhidi ya timu ya Mawezi itakayofanyika Agosti 12 kwenye Uwanja wa Jamhuri Morogoro na wasanii mbalimbali wanatarajiwa kutumbuiza ambao baadhi yao ni pamoja na Juma Nature, Afande Sele, Bill Nass, Mr Blue, Gigy Money, Msaga Sumu, Dolo na Rich One.

Habari Kubwa