Yanga: Tutashambulia mwanzo mwisho

17Mar 2017
Faustine Feliciane
Dar es Salaam
Nipashe
Yanga: Tutashambulia mwanzo mwisho
  • ***Kocha Mwambusi adai hakuna cha kuogopa kwenye mchezo wao dhidi ya Zanaco kesho...

KOCHA msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi, amesema kuwa hawana sababu ya kuwaogopa wapinzani wao Zanaco katika mechi ya mnarudiano kwa sababu wamejiandaa kucheza soka la kushambulia muda wote wa mchezo.

KOCHA msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi.

Akizungumza na Nipashe muda mfupi kabla ya kuondoka nchini kuelekea Zambia jana, Mwambusi alisema kuwa huku wakiwa na akiba ya sare ya bao 1-1 waliyoipata katika mechi ya kwanza, wataingia uwanjani kesho kusaka bao la mapema ili kuwachanganya wenyeji.

"Tulitoka sare ya bao 1-1 hapa nyumbani, hatuwezi kucheza soka la kujihami, tutashambulia muda mwingi ili kupata mabao yatakayotuweka kwenye sehemu salama..., tunahitaji ushindi au sare ya zaidi ya magoli mawili," alisema Mwambusi.

Alisema Zanaco ni timu nzuri lakini hilo haliwezi kuwazuia kutimiza lengo lao la kutaka kusonga mbele kwenye michuano hiyo mikubwa kwa ngazi ya klabu barani Afrika.

Aliongeza kuwa wanashukuru baadhi ya wachezaji waliowakosa katika mechi ya kwanza akiwamo kiungo wa kimataifa kutoka Rwanda, Haruna Niyonzima, wamerejea kwenye timu na wataikabili Zanaco katika mechi ya marudiano.

"Mechi ya Jumamosi haitakuwa ngumu kama ilivyokuwa ile ya kwanza, tumeshawajua wapi wana nguvu na idara ipi ni dhaifu, tunaenda kupambana ili kusaka ushindi, hakuna kisichowezekana katika mchezo wa soka," Mwambusi alisema.

Mzambia Obrey Chirwa anatarajiwa kuongoza safu ya washambuliaji kutokana na mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara kuwakosa Donald Ngoma, Amissi Tambwe na Malimi Busungu ambao ni majeruhi.

Yanga ambayo ilisonga mbele katika mashindano hayo kwa ushindi mnono dhidi ya Ngaya nde Mde ya Comoro inahitaji ushindi wowote au sare ya kuanzia mabao 2-2 ili isonge mbele.

Habari Kubwa