Yanga ubingwa kama Leicester

09May 2016
Faustine Feliciane
Nipashe
Yanga ubingwa kama Leicester
  • ...Huo ni ubingwa wa 26 ikiwa imebakiza mechi tatu mkononi za ligi hiyo ya Tanzania Bara inayotarajiwa kumalizika Mei 21.

YAMETIMIA, kipigo cha bao 1-0 ilichopata Simba kutoka kwa Mwadui FC ya mkoani Shinyanga kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jana kiliifanya Yanga itangazwe kuwa mabingwa wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara kwa msimu wa mwaka 2015/16.

Mashabiki wa Yanga wakishangilia ubingwa huku wameshika kikombe 'bandia' jana kwenye Uwanja wa Taifa baada ya Simba kufungwa bao 1-0 na Mwadui FC.

Yanga imetwaa ubingwa huo wa 26 bila kucheza kama ilivyokuwa kwa Leicester City ya England kutokana na pointi zake 68 kutofikiwa na timu nyingine inayoshiriki ligi hiyo hata kama itafungwa mechi zake tatu zilizosalia.

Mechi tatu ambazo Yanga imebakiza na zote itacheza ugenini ni dhidi ya Mbeya City, Ndanda FC (Mtwara) na Majimaji ya Songea mkoani Ruvuma.

Wawakilishi hao pekee wa Tanzania waliobakia kwenye mashindano kimataifa, mwakani wataiwakilisha Bara kwenye michuano ya Klabu Bingwa Afrika wakati Azam FC ambayo jana ilipata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa CCM Kambarage mkoani Shinyanga itapeperusha bendera ya nchi katika mashindano ya Kombe la Shirikisho.

Azam FC inataka tiketi ya kushiriki mashindano hayo kutokana na kufanikiwa kutinga fainali za michuano ya Kombe la Shirikisho (FA) itakayofanyika hivi karibuni dhidi ya mabingwa hao wa Bara.

Simba yenye pointi 58 baada ya kucheza mechi 27 na inaweza kufikisha pointi 67 endapo itashinda mechi zake tatu zilizobaki wakati Azam FC itafikisha pointi 66.

Goli liliipa ubingwa Yanga lilifungwa na Jamal Mnyate dakika ya 73 aliyemalizia pasi ya mshambuliaji Kelvin Sabato baada ya kupokea mpira mrefu uliopigwa na kipa Jackson Abdulrahman.Dakika ya 90 refa ...alimuonyesha Ajib kadi nyekundu baada ya kumchezea vibaya Mnyate.

Simba ; Vincent Angban, Emery Nimubona, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Novaty Lufunga, Juuko Murshid, Justice Majabvi, Peter Mwalyanzi/Brian Majwega (dk 46), Said Ndemla, Hamisi Kiiza / Mussa Hassan 'Mgosi' (dk 84), Hajji Ugando/ Ibrahim Ajib (dk 46) na Mwinyi Kazimoto.

Mwadui FC; Shaaban Kado/ Jackson Abdulrahman (dk 20), Malika Ndeule, David Luhende, Iddy Mobby, Abdallah Mfuko, Jabir Aziz, Hassan Kabunda, Razack Khalfan, Kelvin Sabato/ Salim Hamisi (dk 89), Rashid Mandawa/ Julius Mrope (dk 69) na Jamal Mnyate.

Habari Kubwa