Yanga uhakika 90%

15Mar 2017
Faustine Feliciane
Dar es Salaam
Nipashe
Yanga uhakika 90%
  • ***Lwandamina asema hakuna kinachoshindikana Zambia, watawanyamazisha wanaosema...

WAKATI Yanga ikijiandaa kuondoka nchini kesho kuelekea Zambia kwa ajili ya mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Zanaco, Kocha George Lwandamina anaamini kwa asilimia kubwa watashinda baada ya kueleza "hakuna kinachoshindikana" katika mechi hiyo.

Lwandamina, alisema jana kuwa wapo wanaoona kama Yanga imeshaondolewa kwenye michuano hiyo kutokana na sare ya bao 1-1 waliyoipata katika mechi ya kwanza iliyochezwa Uwanja wa Taifa Jumamosi iliyopita.

"Mimi nasema tutawanyamazisha wote ambao wameiondoa Yanga kwenye michuano hii..., hakuna kinachoshindikana kwenye soka, tuna uwezo wa kupata ushindi ugenini na ndicho tunachojiandaa nacho," alisema Lwandamina.

Kauli ya Kocha huyo iliungwa mkono na nahodha wake, Nadir Haroub 'Cannavaro' ambaye alisema bado kazi haijaisha na wanaenda kuiondoa Zanaco kwenye mashindano hayo.

"Bado kazi haijaisha..., tuna nafasi ya kusonga mbele, tunaenda Zambia kupambana na mashabiki wasiwe na hofu, mashabiki wanapaswa kutuunga mkono na ikiwezekana twende wote Zambia," alisema Cannavaro.

Yanga inahitaji ushindi au sare ya kuanzia mabao 2-2 ili iweze kusonga mbele kufuatia sare ya nyumbani ya bao 1-1 waliyoipata kwenye Uwanja wa Taifa.

Yanga itaondoka kesho kwa ndege ya Shirika la Ndege la Kenya [Kenya Airways], kuelekea Zambia kwa ajili ya mchezo huo utakaochezwa Jumamosi ijayo.

Habari Kubwa