Yanga wapata kasi ya Biashara

06Dec 2018
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Yanga wapata kasi ya Biashara

IKIWA inaongoza katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga imeanza maandalizi kwa ajili ya kuhakikisha inaondoka na pointi tatu muhimu kwenye mechi dhidi ya Biashara United itakayochezwa Jumapili katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

kocha mkuu wa yanga Mwinyi Zahera, picha na mtandao

Katika kujiandaa na mechi hiyo, jana jioni Yanga inayofundishwa na Mwinyi Zahera ilishuka dimbani kusaka kasi mpya kwa kuwakabili wenyeji Sumbawanga United katika mchezo wa kirafiki uliopigwa Sumbawanga mjini.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mratibu wa Yanga, Hafidh Saleh, alisema benchi la ufundi la timu hiyo linaendelea kuwaimarisha wachezaji wake kwa sababu wanahitaji kuendelea kushinda katika kila mechi wanayocheza.

Saleh alisema wachezaji waliobaki jijini Dar es Salaam wanaendelea na mazoezi maalumu huku wakikumbushwa kuwa hakuna mchezaji mwenye namba ya kudumu katika kikosi cha kwanza.

"Akili zetu ni kuifikiria Biashara United, ni timu mpya kwenye ligi, ila tutawaheshimu kama tulivyofanya kwa timu nyingine, kwa sasa tuko Sumbawanga na leo (jana) jioni tutacheza na Sumbawanga United, baada ya hapo kesho (leo) mchana tutarudi Dar es Salaam kupitia Songwe," alisema mratibu huyo.

Yanga yenye pointi 38 ndiyo inaongoza ligi ikifuatiwa na Azam wenye pointi 36 wakati mabingwa watetezi, Simba wako katika nafasi ya tatu wakiwa na pointi 27, lakini wana mechi mbili mkononi.

Habari Kubwa