Yanga wapigiwa mbiu ya kuchangishana

12Jun 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Yanga wapigiwa mbiu ya kuchangishana

WANACHAMA na mashabiki wa Yanga wamesisitizwa kujitokeza kwa wingi katika harambee ya kuchangia klabu yao ambayo inatarajiwa kufanyika Jumamosi kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam, imeelezwa.

Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela, alisema jana kuwa wanahitaji kuona mwitikio mkubwa katika harambee hiyo ili waweze kutimiza malengo ya kukusanya fedha kwa ajili ya kuwasajili wachezaji wenye ubora watakaoitumikia timu yao katika msimu ujao.

Mwakalebela alisema mchakato wa kusajili wachezaji kwa ajili ya msimu ujao haujakamilika, na kinachokwamisha ni kukosekana kwa fedha klabuni hapo.

"Tunahitaji kupata fedha ili tusajili wachezaji wazuri ambao wataitumikia kwa ushindani klabu yetu, hatutaki kuona msimu ujao tunapoteza mwelekeo, tunawaomba Wana-Yanga kutoka sehemu mbalimbali hapa nchini kujitokeza kwa wingi au kuichangia klabu kwa njia zilizoelekezwa," alisema Mwakalebela.

Aliongeza kuwa, endapo wataimarisha ushirikiano, anaamini malengo ya kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao pamoja na mataji mengine yatatimia.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Hamasa, Anthony Mavunde, alisema wanawashukuru wadau wote wanaoendelea kuichangia Yanga pamoja na wasanii wa muziki na bongo movie wanavyoendelea kuhamasisha ili watu wafike kwenye harambee hiyo.

"Mbali na kufanya harambee hii kubwa kuliko, pia hapo baadaye tutajipanga kupitia wasanii hawa wafanye tamasha maalumu la kuichangia klabu," Mavunde alisema.

Alikitaja kiingilio cha chini katika tamasha hilo litakalofanyika kuanzia saa 4:00 asubuhi hadi saa 10:00 jioni kuwa ni Sh. 50,000.

Baada ya uongozi mpya wa klabu hiyo kuingia madarakani ulitangaza kumkabidhi Kocha Mkuu, Mwinyi Zahera, kiasi cha Sh. bilioni mbili kwa ajili ya kusajili wachezaji wapya ambao wanawahitaji katika msimu ujao.

Habari Kubwa