Yanga watumia ubingwa kuinanga Simba

12May 2016
Joseph Kapinga
Nipashe
Yanga watumia ubingwa kuinanga Simba
  • ***Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limewapa pongezi rasmi za kutwaa ubingwa huo na kuzishukuru timu nyingine 15 zilizoshiriki ligi hiyo..

UBINGWA wa Yanga kabla ya msimu kumalizika umezidi kuwatia jeuri, huku pia wakitumia fursa hiyo kuwananga wapinzani wao Simba, ambao sasa ni msimu wa nne hawajaonja utamu wa taji Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara.

kikosi cha yanga

Mwanzoni mwa wiki hii baada ya mchezo wa ligi dhidi ya Mbeya City kwenye Uwanja wa Sokoine, mjini hapa, Msemaji wa Yanga, Jerry Muro alisema ubingwa wao msimu huu ni wa pekee na aina yake, kwa sababu wameutwaa wakiwa na rekodi ya kuifunga Simba mechi zote mbili.

Muro alisema wameshawahi kutwaa ubingwa mara kadhaa lakini ikiwa ni bila kuifunga Simba, msimu huu hali ilikuwa tofauti kwa kupata pointi sita kutoka kwa watani zao.

"Ubingwa wa mwaka huu ni mtamu kweli kweli, tumeinyoa Simba nyumbani na ugenini," alitamba Muro.

Aliongeza kwamba ushindi katika mechi hizo mbili dhidi ya Msimbazi zilianza kuwapa faraja mapema ya kutimiza malengo yao ya kutwaa ubingwa kabla ya mwisho wa msimu.

Katika mechi ya juzi, Yanga ilishinda mabao 2-0, shukrani kwa beki, Vincent Bossou aliyefunga kipindi cha kwanza na lile la mshambuliaji aliye katika kiwango cha juu waliyemsajili akitokea Simba, Amissi Tambwe la kipindi cha pili.

Ushindi huo uliifanya Yanga kufikisha pointi 71 wakiwa wamebakiza mechi dhidi ya Ndanda FC kwenye Uwanja wa Taifa na ya mwisho dhidi ya Majimaji.

Wapinzani wao Simba, jana walikuwa uwanjani mjini Songea kucheza dhidi ya Majimaji katika mchezo wenye taswira ya kukamilisha ratiba na kulinda heshima.

Yanga ilitangazwa kuwa mabingwa wapya baada ya Simba kukubaki kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Mwadui na kupoteza nafasi ya kutwaa ubingwa baada ya pointi zao 68 (kabla ya mechi ya Mbeya City) kutofikiwa na timu nyingine.

TFF WAIPONGEZA

Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi jana aliipongeza timu hiyo kwa kutwaa ubingwa wa Bara kwa mara ya pili mfululizo baada ya kufanya hivyo msimu uliopita wa mwaka 2014/15.

Malinzi alisema ubingwa huo wa Yanga ni wa 26 ambayo kwa sasa inacheza mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

“Nichukue nafasi hii kuipongeza Yanga kwa ubingwa. Pia nizipongeze timu zote za Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kushiriki na kufanya msimu wa Ligi Kuu Bara 2015/16 kuwa wenye mafanikio,” alisema Malinzi.

Yanga ndiyo inaongoza kwa kutwaa taji hilo mara nyingi tangu ilipoanzishwa mwaka 1965 ikifuatiwa na Simba iliyobeba kikombe mara 18.

Habari Kubwa