Yanga yaahidi kisasi Ngao ya Jamii

29Jul 2021
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Yanga yaahidi kisasi Ngao ya Jamii

BAADA ya kuchapwa bao 1-0 kwenye mechi ya fainali ya Kombe la FA dhidi ya Simba, klabu ya Yanga imewaahidi wanachama na mashabiki wake kuwa italipiza kisasi kwenye mechi ya ufunguzi wa msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2021/22.

Nahodha wa timu hiyo, Bakari Mwamnyeto, amesema kuwa baada ya kupoteza mechi ya fainali dhidi ya Simba na kumalizika kwa msimu bila kupata ubingwa, wanajipanga vema kwa msimu ujao ili kulipiza kisasi cha kufungwa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika na kulikosa kombe la FA.

"Tunashukuru Mungu ligi imeisha salama. Lakini tunajipanga vizuri kwa msimu utakaoanza. Tuko vizuri, tunawaahidi wanachama na mashabiki wa Yanga kuwa hatutowaangusha kwenye mechi ya Ngao ya Jamii," alisema nahodha huyo.

Simba na Yanga zitafungua msimu mpya wa Ligi Kuu 2021/22 kwenye mechi ya Ngao ya Jamii.

"Tutalipiza kisasi na pia tutachukua ubingwa. Hata msimu huu lengo letu lilikuwa ni hilo, lakini ilishindikana, kwa hiyo tunajipanga tena kwa msimu ujao," alisema Mwamnyeto ambaye alisajiliwa kabla ya msimu huu, akitokea Coastal Union.

Kwenye Ligi ya Mabingwa, Mwamnyeto alisema kuwa watajipanga vema ili kufanya vizuri kwenye michuano hiyo pia.

"Hata kwenye mechi za kimataifa, pia tunakwenda kujiandaa kisawasawa ili kuiwakilisha vizuri nchi na naamini tutafanya vema," alisema.

Yanga imemaliza msimu huu ikiwa na Kombe la Mapinduzi pekee ililolitwaa Zanzibar Janauri 13, mwaka huu, baada ya kuichapa Simba kwa mikwaju 4-3 ya penalti, zikitoka suluhu bila kufungana dakika 90 za mchezo.