Yanga yaanza kambi mapema

28Jun 2017
Faustine Feliciane
Dar es salaam
Nipashe
Yanga yaanza kambi mapema

UONGOZI wa klabu ya Yanga umesema kuwa timu hiyo itaingia kambini Julai 4, mwaka huu kwa ajili ya kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kukamilisha usajili wao.

Aidha, klabu hiyo inategemea kutangaza wachezaji iliyowasajili kabla ya kuingia kambini.

Meneja wa klabu hiyo, Hafidha Saleh, aliliambia Nipashe kuwa timu hiyo itaanza maandalizi ya msimu mpya mwanzoni mwa Julai.

"Suala la usajili linafanyiwa kazi na kamati husika, lakini timu itaingia kambini Julai 4 kujiandaa na msimu ujao wa Ligi Kuu pamoja na mashindano mengine," alisema Hafidh.

Aidha, alisema wachezaji ambao wamesajiliwa na wanaotakiwa na klabu hiyo watatangazwa pindi muda wa kufanya hivyo utakapofikia.

Yanga inaelezwa kuwa tayari imemalizana na mshambuliaji wa Simba anayemaliza mkataba wake, Ibrahimu Ajibu na tayari wamempa mkataba wa miaka miwili kuitumikia timu hiyo.

Wakati Ajibu akielezewa kusaini Yanga, Simba tayari ina uhakika wa kumpa mkataba kiungo mahiri wa Yanga na nahodha wa timu ya Taifa ya Rwanda, Haruna Niyonzima, ambaye atasaini mkataba wa miaka miwili pindi akirejea nchini akitokea Rwanda alipokwenda kwa mapumziko ya Sikukuu ya Iddi.

Habari Kubwa