Yanga yaanza viporo kwa ushindi

04Apr 2016
Na Waandishi Wetu
Nipashe
Yanga yaanza viporo kwa ushindi
  • ***Wakati mabingwa watetezi wakianza ratiba ngumu ya mechi za viporo kwa ushindi, Azam yakwama kwa Toto Africans

MABINGWA Yanga waliolalamika kupangiwa ratiba ngumu ya mechi za viporo vya Ligi Kuu Bara, jana walianza vizuri kwa kuwanyoosha Kagera Sugar waliocheza sehemu kubwa ya kipindi cha pili wakiwa 10 kwa kuifunga mabao 3-1 katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

amiss tambwe (mbele), akishangilia bao pamoja na donald ngoma wakati wa mechi dhidi ya kagera sugar.

Wakati Yanga ikitumbukiza kwenye kapu lake pointi tatu muhimu, Azam FC ambao pia jana walianza kushughulikia ratiba ya mechi za viporo, walilazimishwa sare ya 1-1 na Toto Africans ya Mwanza kwenye Uwanja wa CCM Kirumba.

Yanga na Azam zilikuwa nyuma ya ratiba kutokana na kuwa na jukumu la kuiwakilisha nchi kwenye michuano ya Klabu Afrika.

Katika mtanange uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Kagera Sugar ilikuwa ya kwanza kupata bao katika dakika ya 9, likiwa bao la mapema zaidi kufungwa Yanga msimu huu kupitia kwa Mbaraka Yusuph aliyeisindikiza kwenye kamba krosi ya beki wa zamani Simba, Salum Kanoni.

Mabingwa Yanga, walilazimika kusubiri hadi dakika ya 25 kufunga bao la kusawazisha kupitia kwa Donald Ngoma aliyeuweka nyavuni mpira kwa kichwa akimaliza kibarua kizuri cha beki, Juma Abdul.

Yanga wangeweza kubadilisha matokeo kama siyo Kelvin Yondani kukosa penalti iliyochezwa na kipa wa kagera Sugar, Andrew Ntala.

Mwamuzi wa mchezo huo, Erick Unoka kutoka Shinyanga kutoa adhabu hiyo baada ya beki wa Kagera Sugar, Shabani Ibrahim kumkwatua Ngoma ndani ya boksi la hatari.

Yanga ilipoteza nafasi mbalimbali za kufunga kupitia kwa Simon Msuva na Amissi Tambwe kwa kutokuwa makini na mashuti yao kupaa nje ya lango na kuzifanya timu hizo kumaliza nusu ya kwanza zikitoshana nguvu ya bao 1-1.

Mchezaji wa Kagera Sugar alionyeshwa kadi nyekundu kwa mchezo mbaya dhidi ya Ngoma katika dakika ya 47 na kuiacha timu yake kucheza pungufu muda wote wa kipindi cha pili.

Yanga ilitumia vizuri mwanya huo kwa kufunga mabao mawili, la kwanza likiwekwa kwenye kamba na Amisi Tambwe aliyefikisha mabao 18 msimu baada ya kuunganisha krosi ya Msuva, kabla ya Haji Mngwali kufunga bao la tatu katika dakika ya 89.

Mjini Mwanza, Toto Afrika ya jijini Mwanza iliibana Azam FC na kwenda nayo sare ya bao 1-1.
Azam walikuwa wa kwanza kufunga bao kupitia kwa John Bocco dakika ya 23, kabla ya Toto kusawazisha kupitia kwa Waziri Juma.

Katika mechi nyingine, Ndanda walilazimishwa sare ya bila kufungana na Prisons, huku JKT Ruvu wakiifunga African Sports bao 1-0.

Imeandikwa na Somoe Ng'itu (Dar), Daniel Mkate (Mwanza) na Juma Mohamed (Mtwara).

Habari Kubwa