Yanga yachafua hewa CAF

13Oct 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Yanga yachafua hewa CAF

WAKATI wawakilishi wa nchi kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika, Simba, Azam FC na Biashara United wakitarajia kushuka dimbani katika viwanja tofauti ndani na nje ya nchi wiki hii, Yanga imekumbana na rungu zito kutoka Shirikisho la Soka Afrika, CAF.

Ijumaa wiki hii, Biashara United itakuwa mwenyeji wa Al Ahli Tripoli ya Libya katika mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika itakayopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, wakati Jumamosi Azam FC ikiikaribisha Pyramids ya Libya uwanjani hapo kwenye michuano hiyo.

Mabingwa wa nchi, Simba wenyewe Jumapili watakuwa ugenini nchini Botswana kuwavaa Jwaneng Galaxy kwenye mechi ya raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika kabla ya kurudiana Oktoba 24, mwaka huu katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam na timu itakayopata ushindi wa jumla itatinga hatua ya makundi ya michuano hiyo.

Kwa upande wa Azam FC na Biashara United kama zikipata matokeo ya jumla kwenye mechi ya nyumbani na ugenini, basi zitalazimika kusubiri kupangiwa timu zitakazotolewa kwenye raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa ili kucheza mechi moja ya mtoano nyumbani na ugenini kuwania kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho.

Hata hivyo, wawakilishi hao wa nchi watapaswa kuwa makini kwa kufuata kanuni na taratibu zote zilizowekwa na CAF ili kuiepusha Tanzania kutoangukia adhabu kali kutoka shirikisho hilo, baada ya TFF kupewa onyo kutokana na tukio la hivi karibuni lililofanywa na Klabu ya Yanga na mengine ya nyuma.

Yanga ilikuwa ikiiwakilishi nchi kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu, kabla ya kutolewa na Rivers United katika hatua ya awali kwa jumla ya mabao 2-0 baada ya kufungwa bao 1-0 nyumbani na ugenini.

Hata hivyo, katika mchezo wa awali kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, baadhi ya mashabiki wa Yanga walionekana wakiwafanyia vurugu viongozi wa Rivers United kwa kuwapiga.

Hivyo, hivi karibuni Kamati ya Nidhamu ya CAF, iliipiga faini Yanga ya dola za Kimarekani 5,000 sawa na Shilingi 11,521,900 za Tanzania kutokana na Klabu ya Rivers United kuripoti matukio ya kufanyiwa vurugu pamoja na kuonekana baadhi ya mashabiki katika mchezo huo wa Ligi ya Mabingwa Afrika ambao ulitakiwa kuchezwa bila ya mashabiki.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Ofisa Habari na Mawasiliano wa TFF, Cliford Ndimbo, ilieleza kuwa pamoja na Yanga kupata taarifa ya malalamiko ya Rivers United sambamba na uamuzi wa CAF kupitia TFF, lakini haikujibu chochote.

"Pia Tanzania imepewa onyo kutokana na kuripotiwa kwa matukio mengi kwenye vyumba vya kubadili nguo pale klabu za hapa nchini zinapocheza mashindano ya kimataifa na masuala ya vipimo vya PCR vya Uviko-19 (COVID-19)," ilieleza taarifa hiyo.

Kutokana na uzito wa suala hilo, TFF imezitaka klabu kuheshimu na kufuata kanuni, utaratibu na maelekezo ya CAF.

Aidha, kutokana na tatizo hilo imeilazimu TFF kukutana mara moja na klabu zinazoshiriki mashindano ya kimataifa Simba, Azam na Biashara United ili kufanyia kazi kasoro zote zilizojitokeza katika michezo ya awali.

Habari Kubwa