Yanga yachana Mbao Kirumba

23Oct 2019
Adam Fungamwango
Mwanza
Nipashe
Yanga yachana Mbao Kirumba
  • ***Ushindi huo waongeza molari ya kuwakaribisha Pyramids hapo Jumapili...

BAO pekee lililofungwa na Mnamibia Sadney Urikhob liliiwezesha Yanga kuibuka na ushindi katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mbao FC, iliyochezwa jana kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Kwa matokeo hayo, Yanga ambayo imecheza mechi nne, imefikisha pointi saba sawa na Mbao FC, lakini imepanda hadi katika nafasi ya 10 kwenye msimamo wa ligi hiyo huku wenyeji wao wakibakia katika nafasi ya 13.

Urikhob alifunga bao hilo akiwa ndani ya eneo la hatari, akiwa amezungukwa na mabeki watano wa Mbao, ambao walizembea kuuokoa mpira au na kumfanya mfungaji huyo wa Yanga kugeuka na kuupiga mpira kwa mguu wake wa kushoto ambao kipa, Abdallah Makangame, alishindwa kuudaka na kutinga wavuni.

Kipindi cha kwanza, Mbao FC haikufanya shambulizi lolote la maana, badala yake ilijaza viungo kati na mabeki nyuma kwa ajili ya kulinda zaidi lango kuliko kushambulia, huku wakimwacha Said Hamisi mbele bila ya kuwa na msaidizi.

Badala yake Yanga ambayo tena haikuwa na Kocha Mkuu, Mwinyi Zahera, katika benchi, ilikuwa ikijitahidi kupeleka mbele mashambulizi lakini, washambuliaji wake walishindwa kutumia vema nafasi tatu za wazi walizozitengeneza kwa kukosa utulivu.

Dakika ya nane tu ya mchezo, Feisal Salum alipiga shuti kubwa juu, alipopata nafasi safi iliyotokana na kutokea kizaazaa kwenye lango la Mbao FC huku dakika ya 11, David Molinga akiwa kwenye eneo zuri, aliachia shuti kali lililodakwa na kipa Makangame.

Dakika ya tatu ya nyongeza, kabla ya kukamilika kwa kipindi cha kwanza, mpira wa kichwa uliopigwa na nahodha wa Yanga, Papy Tshishimbi, uligonga mwamba wa juu kutokana na krosi safi iliyopigwa na Juma Abdul na kuikosesha Yanga bao la kuongoza kabla ya mapumziko.

Kipindi cha pili mpira ulichangamka zaidi na pamoja na Urikhob kuipatia Yanga bao pekee, lakini alikosa magoli mengine mawili, dakika ya 49 kabla ya kufunga goli, na dakika ya 72.

Mbao ilipoteza nafasi mbili za kusawazisha bao dakika za mwisho wa mchezo, 82 na 86, lakini straika wake wa kutegemewa, Said Hamisi alikosa utulivu na Frank Shikalo kuokoa hatari hizo.

Pamoja ya Mbao kumwingiza straika wa zamani wa Toto African, Azam FC na Biashara United Waziri Junior, lakini hakuwa na msaada wowote hadi dakika 90 zilipomalizika.

Katika mechi nyingine ya Ligi Kuu Bara iliyochezwa kwenye Uwanja wa Uhuru, JKT Tanzania ilitoka suluhu dhidi ya KMC FC, zote za jijini hapa.

Ligi hiyo inatarajia kuendelea tena leo kwa mabingwa watetezi, Simba kuvaana na Azam FC kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam huku Polisi Tanzania wakiwakaribisha Mwadui FC kwenye Uwanja wa Chuo cha Ushirika mjini Moshi.

Habari Kubwa