YANGA YACHANUA, SIMBA YAPIGWA

07Nov 2016
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
YANGA YACHANUA, SIMBA YAPIGWA
  • ***Msuva aipaisha ugenini kwa tuta, mfumo wamgharimu Omog Uhuru wakati Azam nayo ikichezea kichapo...

WAKATI Yanga ikiibuka na ushindi wa bao 1-0 katika Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, watani wao Simba wamepunguzwa kasi baada ya kufungwa idadi kama hiyo na African Lyon katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara uliopigwa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Katika mchezo huo uliochezeshwa na Ahmada Simba wa Kagera, aliyesaidiwa na Soud Lilla na Frank Komba wote wa Dar es Salaam, shujaa wa Lyon alikuwa ni ‘kinda’ Abdallah Mguhi aliyefunga bao hilo pekee dakika za majeruhi akimalizia krosi ya Miraj Adam kutoka kulia.

Katika dakika 45 za kipindi cha kwanza timu hizo zilishambuliana kwa zamu, lakini leo Simba hawakuwa katika ubora kutokana na mfumo uliotumiwa na kocha Mcameroon, Joseph Marius Omog akianzisha viungo watano na mshambuliaji mmoja tu, Mrundi Laudit Mavugo ambaye alishindwa kufurukuta.

Beki Mkongo Janvier Besala Bokungu alikaribia kuifungia Simba dakika ya 19 baada ya kupiga shuti ambalo kipa Mcameroon wa Lyon, Rostand Youthe alidaka.

Beki Miraj Adam alikaribia kuiadhibu timu yake ya zamani dakika ya 39 baada ya kupiga shuti la mpira wa adhabu lililogonga mwamba wa lango na kutoka nje.

Kipindi cha pili Omog alianza kwa kuiongezea makali safu ya ushambuliaji akimtoa kiungo Mohammed ‘Mo’ Ibrahim na kumuingiza mshambuliaji Ibrahim Hajib.

Angalau kidogo Simba ikaanza kulitia misukosuko lango la African Lyon, ambayo sehemu kubwa ya kipindi cha pili ilicheza mchezo wa kujihami ikitumia mashambulizi ya kushtukiza.

Kwa matokeo hayo, Simba inabaki na pointi zake 35 baada ya kucheza mechi 14, lakini inaendelea kuongoza Ligi Kuu mbele ya mabingwa watetezi, Yanga wenye pointi 30 za mechi 14 pia.

Kikosi cha African Lyon kilikuwa; Rostand Youthe, Miraj Suleiman, Baraka Jaffar, Hamad Waziri, Isihaka Hassan, Omar Salum, Awadh Juma, Khalfan Twenye/Rehani Kibingu dk 88, Hamad Manzi/Amani Peter dk 63, Abdallah Mguhi ‘Messi’ na Omar Abdallah.

Simba SC; Vincent Angban, Janvier Bokungu, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Novaty Lufunga, Method Mwanjali, Jonas Mkude, Shizza Kichuya, Muzamil Yassin, Mohamed ‘Mo’ Ibrahim/Ibrahim Hajib dk 50, Laudit Mavugo/Said Ndemla dk 81 na Mwinyi Kazimoto/Jamal Mnyate dk 76.

MBEYA
Yanga iliibuka ilipata bao lake kwa njia ya penalti katika dakika ya 70 kupitia kwa Simon Msuva.
Penalti hiyo ilitokana na Deus Kaseke kuangushwa nadani ya boksi na Victor Hangaya.

Kwingineko

Azam FC jana ilichezea kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Mbao FC ambayo iliutumia vema uwanja wake wa nyumbani wa CCM Kirumba.

Nayo Kagera Sugar ilikubali kipigo cha mabao 3-1 kutoka kwa JKT Ruvu.

Habari Kubwa