Yanga yaendelea kumwota Morrison

21Nov 2020
Saada Akida
Dar es Salaam
Nipashe
Yanga yaendelea kumwota Morrison

WAKATI uongozi wa Yanga ukimtangaza, Haji Mfikirwa kuwa Kaimu Katibu Mkuu wao, klabu hiyo imelitaka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kusikiliza shauri na malalamiko yao kuhusiana na mkataba wa winga mshambuliaji wa Simba, Bernard Morrison.

Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela, picha mtandao

Mfikirwa amechukua mikoba ya Simon Patrick ambaye amesimamishwa na mabosi wa klabu hiyo ili kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela, alisema wanaiomba TFF kukutana na kujadili kesi ambazo ziliwasilishwa na klabu yao kabla ya dirisha dogo la usajili halijafunguliwa ifikapo Desemba 15, mwaka huu.

Mwakalebela aliitaja kesi nyingine ambayo wanahitaji itolewe uamuzi ni kuhusiana na tuhuma zilizowekwa wazi na golikipa wao, Ramadhani Kabwili, ambaye klabu mojawapo ilitaka kumlaghai.

"Tuna wasiwasi dirisha la usajili likifunguliwa watatumia nafasi hiyo kupeleka mkataba uliokamilika katika mtandao," alisema Mwakalebela.

Aliongeza Yanga inajipanga kukabiliana na hujuma mbalimbali wanazofanyiwa ili wafikie malengo yao ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

Naye Mshauri wa Yanga, Senzo Mbatha alisema kikosi cha Yanga kiko vizuri, lakini kuelekea mchezo wao wa kesho dhidi na Namungo FC, watamkosa kiungo wao wa kimataifa kutoka Rwanda, Haruna Niyonzima.

"Nimezungumza na Kocha, Cedric Kaze, amehakikisha kikosi kipo vizuri, Niyonzima hatakuwapo, alienda Rwanda na alipata ajali, lakini hakupata majeraha yoyote na anaendelea vizuri," alisema Senzo.

Kuhusu suala la mchakato wa mabadiliko, alisema unaendelea vizuri na kati ya Jumatatu na Jumanne wanatarajia wawakilishi wao wawili kwenda Hispania kuchukua ripoti ya mfumo huo ilipofikia.

Aliongeza tayari klabu hiyo imetangaza zabuni kwa ajili ya ujenzi wa hosteli na uwanja wa mazoezi utakaojengwa katika eneo la Kigamboni jijini, Dar es Salaam.

Habari Kubwa