Yanga yaendeleza makali Morogoro

20Jul 2019
Shufaa Lyimo
Dar es Salaam
Nipashe
Yanga yaendeleza makali Morogoro

YANGA imeendelea kufanya vema katika mechi zake za kirafiki baada ya kupata ushindi wa pili mfululizo kwa kuwafunga Moro Kids mabao 2-0 katika mchezo wa kirafiki uliochezwa jana kwenye Uwanja wa Highland Parks mkoani Morogoro.

Mabao ya Yanga katika mchezo huo wa jana yalifungwa na Mganda Juma Balinya aliyefunga kwa njia ya penalti huku lingine likipachikwa na Paul Godfrey.

Mratibu wa Yanga, Hafidh Saleh, alisema jana kuwa wachezaji wa timu hiyo wameendelea kuonyesha ushindani katika mchezo huo ambao Kocha, Noel Mwandila, aliendelea kutoa nafasi mbalimbali kwa nyota wa mabingwa hao wa historia.

"Mechi ilikuwa nzuri, wachezaji wameendelea kuonyesha ukomavu na kila mmoja anataka kujihakikisha nafasi kwenye kikosi cha kwanza, wanataka kuwa imara kabla ya Kocha Mkuu, Mwinyi Zahera hajafika kambini hapo," alisema Saleh.

Katika mchezo wa kwanza wa kirafiki uliochezwa mkoani humo, Yanga ilipata ushindi wa mabao 10-1 dhidi ya Tanzanite Academy.