Yanga yafanya kweli Ligi Kuu

09Nov 2019
Isaac Kijoti
Mtwara
Nipashe
Yanga yafanya kweli Ligi Kuu
  • **Yaifunga Ndanda bao 1-0 ndani ya Nangwanda, lakini gonjwa la Zahera lamtesa Mkwasa...

MRITHI wa Mwinyi Zahera, Boniface Mkwasa "Master", ameanza kazi yake vema ya kuiongoza Yanga baada ya kuwafurahisha mashabiki na wanachama wa timu hiyo kwa kuipa ushindi dhidi ya wenyeji Ndanda FC jana.

Katika mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini hapa, Yanga iliibuka na ushindi wa bao 1-0, shukrani zikimwendea Mnyarwanda Patrick Sibomana aliyezamisha kimyani mpira wa faulo dakika ya 75.

Huo ni ushindi wa tatu kwa Yanga msimu huu na wa kwanza kwa Mkwasa tangu alipokabidhiwa mikoba ya kuinoa timu hiyo Jumanne wiki hii baada ya 'ndoa ya Zahera na klabu hiyo' kuvunjika.

Aidha, ushindi huo unaifanya Yanga kufikisha pointi 10 baada ya kushuka dimbani mara tano ikipoteza mchezo mmoja na kutoka sare moja.

Hata hivyo, gonjwa la safu ya ushambuliaji kukosa umakini tangu ikiwa chini ya Zahera kwa kutegemea kupata mabao kwa kutumia mipira iliyokufa ndilo lililoonekana kumtesa Mkwasa na sasa itabidi kulifanyia kazi.

Katika kipindi cha kwanza licha ya Yanga kumiliki mpira kwa asilimia kubwa haikuweza kutumia vema nafasi ilizotengeneza katika mchezo huo, tatizo likionekana kuwa lile lile la safu ya ushambuliaji kukosa umakini na hivyo kushindwa kutumia vizuri nafasi mbalimbali inazotengeneza na kuwapa presha mashabiki wao.

Pamoja na hali ya Uwanja wa Nangwanda kutokuwa rafiki, lakini kama Yanga ingekuwa makini kwa faulo ya dakika ya 33 iliyopigwa na David Molinga, mambo yangeweza kuwa tofauti.

Kadhalika, Molinga alichezewa faulo na Samweli Mahulo dakika ya 43 lakini safari hii Juma Abdul alishindwa kuitendea haki na Yanga kukosa bao.

Kwa ujumla kucheza kwa nidhamu na umakini kwa mabeki wa Ndanda huku Yanga ugonjwa wao wa kutokuwa watulivu katika safu ya ushambuliaji ndilo lililoendelea kuwa tatizo la kukosa mabao kipindi cha kwanza.

Lakini pia tatizo la Ndanda kulinda zaidi huku wakishindwa kucheza kwa mashambulizi ya kushtukiza kuliwaacha huru zaidi mabeki wa Yanga na kuruhusu mashambulizi kwao ambayo hayakuwa na madhara kutokana na ubutu wa safu ya ushambuliaji wa wapinzani wao.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku Ndanda ikijilinda zaidi na kusababisha mashambulizi mengi langoni mwao huku Deus Kaseke akionekana kuwa mwiba mkali kwao, lakini madhara yake makubwa yalikuwa dakika ya 51 ambapo shuti lake litoka nje.

Dakika ya 59, Sibomana alishindwa kuwa makini kulenga lango baada ya kushindwa kuitendea haki krosi ya Kaseke lakini kuingia kwa Mrisho Ngassa dakika ya 64 akichukua nafasi ya Rafael Daudi kulizaa matokeo chanya baada ya kufanyiwa faulo dakika ya 74 iliyopigwa na Molinga kabla ya mwamuzi kuamuru irudiwe na safari hii ikipigwa na Sibomana aliyefunga bao na kuifanya timu hiyo ipate pointi tatu muhimu katika mchezo huo.

Licha ya Ndanda kuhaha ikitaka kusawazisha safu ya ulinzi ya Yanga ikiwa chini ya Kelvin Yondani ilikuwa makini huku kiungo cha kati kikiifanya kazi yake vema kwa kukabia kati.

Habari Kubwa