Yanga yafikiria makundi Afrika

19Jul 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Yanga yafikiria makundi Afrika

WAKATI kikosi cha Yanga kikiwa kinaendelea na mazoezi yake mkoani Morogoro, uongozi wa timu hiyo ya jijini Dar es Salaam umesema kuwa lengo lao kuu ni kuona wanafika hatua ya makundi ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao.

 ​​​​​​​Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela

 Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela, alisema kuwa wamejipanga kufika hatua hiyo au zaidi, licha ya timu yao kupata tiketi ya kushiriki michuano hiyo wakiwa katikati ya mchakato wa usajili.

Mwakalebela alisema kuwa wanaamini watafanya vema kwa sababu baadhi ya wachezaji wao wana uzoefu na mashindano kutokana na kushiriki wakiwa na timu nyingine.

"Tutacheza kwa kuangalia malengo yetu, tunajua tunatakiwa tucheze ligi na wakati huo huo mechi za mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika," alisema Mwakalebela.

Aliongeza pia wanaendelea vema na maandalizi ya tamasha la Siku ya Mwananchi ambalo litafanyika Agosti 4 mwaka huu kwa kushuhudia mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya AS Vita kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).