Yanga yafuata  nyayo za Simba

06Dec 2017
Faustine Feliciane
Nipashe
Yanga yafuata  nyayo za Simba
  • *** Yaitisha mkutano kujadili mabadiliko ya uendeshaji wa klabu…

SIKU chache baada ya Simba kukamilisha mchakato wa mabadiliko ya uendeshaji wa klabu hiyo kuwa kampuni, Yanga nao wameanza mchakato wa kufuata nyayo hizo, imeelezwa.

Wanachama wa Simba inayodhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo Michezoni ya SportPesa, wameridhia mabadiliko hayo ambapo mwanachama wa klabu hiyo na mfanyabiashara maarufu nchini, Mohamed "MO" Dewji ameshinda zabuni ya kununua hisa asilimia 50 za klabu hiyo.

Akizungumza na redio moja ya jijini Dar es Salaam, Kaimu Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga, alisema kimsingi mabadiliko ya uendeshaji wa klabu za soka nchini ni muhimu katika maendeleo ya soka Tanzania.

“Kamati ya Utendaji itakutana Desemba 13, mwaka huu kuanza mchakato wa kufanya mabadiliko ya uendeshaji wa klabu yetu, tutalifikisha hili kwa wanachama,” alisema Sanga.

Sanga alisema mchakato huo katika klabu yao ulianza muda mrefu, lakini ulisimama kwa sababu mbalimbali.

“Katiba yetu ambayo tuliifanyia marekebisho mwaka 2010, inaruhusu mabadiliko haya, lakini hapo awali kulikuwa na suala la kampuni ndani ya klabu kwa maana ya kuwa na klabu kama klabu na pia kuwa na kampuni... hivyo jambo kama hili litazungumzwa kwa wanachama kuona nini tunaamua,” alisema Sanga.

Alisema wataamua kama klabu ijiendeshe kama kampuni au kuwapo kwa kampuni ndani ya klabu ya Yanga ambayo nayo inadhaminiwa na SportPesa.

Alisema wazo la kuwa na kampuni lilikuwapo Yanga kwa miaka ya nyuma, lakini halikuendelezwa kwa sababu mbalimbali.

Sanga, alisema baada ya mkutano huo wa kamati ya Utendaji utaitishwa mkutano wa wanachama kwa ajili ya kuwasilisha hoja hiyo.

Kama Yanga itaanzisha mchakato huo na kufanikiwa kuukamilisha, watakuwa wamekamilisha hatua ambayo Simba wameifikia ya kubadili uendeshaji wa klabu yao kutoka kuwa Simba SC na kuwa Simba SC Limited kwa kuuza hisa za klabu hiyo.

 

Habari Kubwa