Yanga yafuata  kiungo Chalenji

05Dec 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Yanga yafuata  kiungo Chalenji

KAMATI ya Usajili ya Klabu ya Yanga imepanga kwenda kwenye michuano inayoendelea ya Cecafa Chalenji kwa lengo la kusaka mchezaji wa kiungo kwa ajili ya kuimarisha kikosi chao.

Kocha Mkuu wa timu ya Yanga, George Lwandamina

Michuano ya Chalenji inaendelea nchini Kenya ambapo mataifa manane yanaumana kuwania ubingwa wa mashindano hayo.

Mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo inayoongozwa na Hussein Nyika, aliliambia Nipashe kuwa kocha wa timu hiyo inayodhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo Michezoni ya SportPesa, George Lwandamina, ametaka kutafutiwa mchezaji mwenye kiwango cha juu kwenye nafasi ya kiungo wa kati.

Mpenyezaji wa habari hizo, ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, pia ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo, alisema Lwandamina amepanga kusajili kiungo kwa kuwa hana uhakika kama Thaban Kamusoko ambaye amekuwa akiandamwa na majeruhi atarejea kwenye ubora wake mapema.

“Kocha ameleta hili kwenye kamati, wapo wachezaji ambao tunajaribu kuwafuatilia nje ya Afrika Mashariki, lakini pia tunaangazia michuano ya Cecafa kuona kama tutampata mchezaji mwenye viwango ambavyo kocha anavitaka,” alisema Mjumbe huyo.

Aidha, alisema pindi watakapompata watamleta nchini kwa ajili ya majaribio chini ya Lwandamina ambaye ndiye atakayetoa idhini ya kusajiliwa.

Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh, alipoulizwa juu ya mpango huo, alisema suala la usajili lipo mikononi mwa kocha na kamati ya usajili.

“Inawezekana hilo likawapo au la, unajua suala la usajili ni la kocha na Kamati ya Usajili, yapo mapendekezo ya kocha na yanafanyiwa kazi na uongozi,” alisema Saleh.

 

Habari Kubwa